• HABARI MPYA

  Jumanne, Juni 19, 2018

  SERIKALI YAUFUNGIA WIMBO MPYA WA MBUNGE SUGU NA KUMUONYA ASIUSAMBAZE

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA), limeufungia wimbo wa #219 ulioimbwa na Joseph Mbilinyi maarufu Sugu kwa madai una maneno ya uchochezi.
  Wimbo huu umepigwa marufuku ikiwa ni siku chache tangu Sugu ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini autambulishe.
  Kwa mujibu wa taarifa ya Katibu Mtendaji wa BASATA Godfrey Mngereza, wimbo huo umepigwa marufuku kupigwa kwenye vyombo vya habari na mahali pengine popote kwa madai unahatarisha amani na utengamano miongoni mwa jamii.
  Sanjari na kuufungia wimbo huo, BASATA imemuonya Sugu na kumwagiza kuacha kuutangaza au kuusambaza wimbo huo.
  Joseph Mbilinyi 'Sugu' ambaye wimbo wake umefungiwa kwa madai una maneno ya uchochezi

  “Ieleweke kwamba kwa mujibu wa kifungu cha 4 (1) (j) cha sheria ya BASATA namba 23, ya mwaka 1984, Baraza limepewa mamlaka ya kuratibu na kufuatilia mienendo ya mtu yeyote anayejihusisha na kazi za sanaa na kuhakikisha inalinda maadili ya kitaifa miongoni mwa wasanii wanapokuwa jukwaani au wanapobuni kazi yoyote ya sanaa.
  “Baraza limekuwa likipokea simu za maswali na malalamiko kadhaa kutoka kwa wadau wa sanaa ambao kwa njia moja au nyingine wameguswa na kuchukizwa na wimbo huu ambao si tu una maneno ya kichochezi, kutofuata taratibu za utoaji wimbo kwa umma bali pia kazi hii inawafanya watu makini kuanza kuhoji hadhi ya msanii, weledi, taaluma na lengo la kazi ya sanaa kwa ujumla,” amesema Mngereza.
  Sugu alitunga wimbo huo na kuupa jina la #219 ikiwa ni namba yake ya mfungwa aliyopewa alipokuwa jela kutumikia kifungo cha miezi mitano alichohukumiwa Februari mwaka huu, kwa kutoa maneno ya kumkashifu Rais John Magufuli, baada ya kutoka kwa msamaha wa Rais Aprili mwaka huu.
  Pia sugu amekuwa akitumia namba hiyo kwa kuitengenezea beji ambayo huibandika katika kola ya suti yake awapo bungeni.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SERIKALI YAUFUNGIA WIMBO MPYA WA MBUNGE SUGU NA KUMUONYA ASIUSAMBAZE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top