• HABARI MPYA

  Jumamosi, Juni 30, 2018

  SALAMBA AFUNGA MABAO MAWILI SIMBA SC IKIWATANDIKA 4-0 WASOMALI KOMBE LA KAGAME

  Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
  TIMU za Tanzania Bara zimeendelea kufanya vizuri katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Kombe la Kagame baada ya leo mchana Simba kushinda mabao 4-0 dhidi ya Dakadaha FC ya Somalia.
  Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Simba ilichezesha wachezaji wake wengi wapya wakiongozwa na Adam Salamba aliyesajiliwa kutoka Lipuli FC.
  Wachezaji wapya wengine walioichezea Simba katika mchezo huo ni Marcel Kaheza aliyesajiliwa kutoka Majimaji SC ya Songea, Pascal Wawa na Mohamed Rashid kutoka Prisons ya Mbeya.
  Katika mchezo huo wa Kundi C, Dakadaha FC hawakuonyesha upinzani mkubwa kwa Simba na kujikuta ikifungwa mabao manne na kushindwa kupata hata bao moja la kufutia machozi.
  Adam Salamba (katikati) akipongezwa na wenzake baada ya kuifungia mabao mawili Simba SC leo

  Salamba ndiye aliyeonekana kuwa mwiba kwa Dakadaha FC baada ya kuifungia Simba mabao mawili katika dakika za 23 na 76 huku Kaheza naye akifunga bao moja dakika ya 18 na Rashid Juma akaifungia Simba bao dakika ya 45.
  Matokeo hayo yameifanya Simba kuongoza katika Kundi C ikiwa na pointi tatu sawa na Singida United lakini yenyewe ina tofauti kubwa ya mabao ya kufunga na kufungwa na haijaruhusu wavu wake kuguswa.
  Singida United ipo nafasi ya pili kwani licha ya kuwa na pointi tatu lakini ina tofauti ya mabao moja wakati Simba ina tofauti ya mabao nne. APR ipo nafasi ya tatu na Dakadaha FC inashika mkia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SALAMBA AFUNGA MABAO MAWILI SIMBA SC IKIWATANDIKA 4-0 WASOMALI KOMBE LA KAGAME Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top