• HABARI MPYA

  Jumatano, Juni 27, 2018

  MWANAFUNZI WA DARASA LA TANO JAMILLAH OMARY ANG'ARA UMITASHUMTA MWANZA

  Na Masau Bwire, MWANZA
  BINTI Jamillah Omary, mwanafunzi wa darasa la tano, shule ya msingi Mbezi-Ndumbwi, Dar es Salaam, mchezaji wa soka la wanawake amekuwa kivutio kikubwa katika mashindano ya UMITASHUMTA yanayoendelea katika viwanja vya chuo cha ualimu, Butimba, Mwanza. 
  Jamillah, msichana mdogo kwa umri na umbo, ameonesha uwezo mkubwa wa kucheza soka na kujipatia umaarufu mkubwa katika mashindano haya, ambapo mashabiki wake wanalazimika kumuita kwa jina la Christian Ronaldo.
  Mchezaji huyo, Jamillah anapokuwa na mpira, huwa na mambo mengi, mbali na kujiamini, ana chenga za mahudhi, ni fundi wa kufunga magoli mazuri, ana akili kubwa ya kucheza soka hali iliyowashawishi mashabiki wake kumuita kwa jina la Ronaldo, wakimlinganisha kwa uwezo wa kucheza mpira. 

  Huyu ndiye Jamillah Omary, mwanafunzi wa darasa la tano, shule ya msingi Mbezi-Ndumbwi, Dar es Salaam anayefanya vizuri katika soka ya wanawake  

  Kutokana na uchezaji wake kuwafurahisha watazamaji, siku ambayo timu ya soka la wanawake, mkoa wa Dar Es salaam inapocheza, mashabiki hufurika uwanjani ili kushuhudia na kuburudika na 'mambo' ya Jamillah uwanjani, mpira unapomalizika, wengi uomba kupiga naye picha wakiwemo waamuzi wa mchezo.
  Jamillah ametoa mchango mkubwa kwa timu yake ya soka la wanawake mkoa wa Dar Es salaam na kuiwezesha kutinga hatua ya fainali katika mashindano hayo ya Umitashumta ambapo, Alhamis, Juni 28, 2018 timu yake itapambana na timu ya mkoa wa Tabora katika hatua hiyo ya fainali. 
  Afisa Elimu Mkoa wa Dar Es salaam, Hamis Lisu, mbali ya kumpongeza kijana huyo, ameiomba TFF kumjumuisha na kumtumia katika timu ya Taifa kwani, alisema kipaji alichonacho kikiendelezwa atakuwa lulu kwa Taifa kwa soka la wanawake, wazo lililoungwa mkono na wadau wa soka akiwemo mwamuzi wa soka, mwanamke, Neema Mwambashi wa Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MWANAFUNZI WA DARASA LA TANO JAMILLAH OMARY ANG'ARA UMITASHUMTA MWANZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top