• HABARI MPYA

  Tuesday, October 03, 2017

  TAIFA STARS KUANZA MAZOEZI BOKO VETERANI KESHO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIKOSI cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kinatarajiwa kuanza mazoezi kesho asubuhi kwenye Uwanja wa Boko Veterani, eneo la Bunju mjini Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya Malawi Jumamosi ijayo.
  Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba kikosi hicho kitafanya mazoezi kwenye Uwanja huo kwa siku tatu kabla ya kuhamia Uwanja wa Uhuru.
  Lucas amesema kwamba wachezaji wanaocheza nje walioitwa kwenye timu hiyo wameanza kuwasili leo na wanatarajiwa hadi kufuka kesho wote sita walioitwa watakuwa wamekwishawasili.  
  Hao ni Morel Orgenes kutoka FC Famalicao ya Ureno, Abdi Banda kutoka Baroka FC ya Afrika Kusini, Hamisi Abdallah kutoka Sony Sugar, Abdul Hilal kutoka Tusker zote za Kenya, Simon Msuva kutoka Difaa Hassan El – Jadidah ya Morocco na Nahodha, Mbwana Samatta kutoka KRC Genk ya Ubelgiji.
  Nahodha Mbwana Samatta anatarajiwa kuwasili usiku huu kutoka Ubelgiji
  Tayari Msuva, mchezaji wa zamani wa klabu ya Yanga yupo nchini, wakati Samatta mchezaji wa zamani wa Simba SC anatarajiwa kuwasili usiku wa leo.
  Kwa ujumla kikosi kiliochoteuliwa na kocha Salum Shaaban Mayanga kwa ajili ya mchezo huo kinaundwa na makipa; Aishi Manula (Simba SC), Ramadhani Kabwili (Yanga) na Peter Manyika (Singida United).
  Mabeki Gardiel Michael (Yanga), Boniphace Maganga (Mbao FC), Abdi Banda (Baroka FC/Afrika Kusini), Kelvin Yondani (Yanga), Salim Mbonde (Simba SC), Erasto Nyoni (Simba SC) na Adeyum Ahmed (Kagera Sugar).
  Viungo ni Himid Mao ambaye pia ni Nahodha Msaidizi (Azam FC), Hamisi Abdallah (Sony Sugar/Kenya), Muzamil Yassin (Simba SC), Raphael Daud (Yanga), Simon Msuva (Difaa El Jadidah/Morocco), Shiza Kichuya (Simba SC), Abdul Hilal (Tusker/Kenya) na Morel Orgenes (FC Famalicao/Ureno).
  Washambuliaji ni Mbwana Samatta (KRC Genk/Ubelgiji), Ibrahim Hajib (Yanga) na Mbaraka Yussuph (Azam FC). 
  Benchi la Ufundi la Mayanga linaundwa na yeye mwenyewe ambaye ni Kocha Mkuu, Fulgence Novatus (Kocha Msaidizi), Ame Ninje (Kocha Msaidizi), Patrick Mwangata (Kocha wa Makipa), Danny Msangi (Meneja), Dkt. Richard Yomba (Daktari wa timu), Dkt. Gilbert Kigadye (Daktari wa Viungo) na Ally Ruvu (Mtunza Vifaa).  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TAIFA STARS KUANZA MAZOEZI BOKO VETERANI KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top