• HABARI MPYA

  Jumamosi, Oktoba 28, 2017

  YANGA YAIVIMBIA SIMBA, SARE 1-1 MABAO YA KICHUYA NA CHIRWA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES ZALAAM
  VIGOGO wa soka nchini, Simba na Yanga leo wamegawana pointi baada ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliofanyika Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
  Kwa matokeo hayo, Simba na Yanga zote zinafikisha pointi 16 baada ya kucheza mechi nane kila moja – maana yake Ligi Kuu msimu imekuwa ya ushindani zaidi, vigogo hao wakichuana na Azam FC na Mtibwa Sugar kileleni. 
  Yanga ndiyo waliolazimika kupigana kusawazisha bao kupitia kwa mshambuliaji wake, Mzambia, Obrey Chirwa baada ya winga Shiza Kichuya kuanza kuwafungia Simba, mabao yote yakipatikana kipindi cha pili.
  Kiungo wa Simba, Mghana James Kotei akimkwatua mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajib
  Mfungaji wa bao la Yanga, Obrey Chirwa akiwatoka wachezaji wa Simba
  Mfungaji wa bao la Simba, Shiza Kichuya akimiliki mpira mbele ya beki wa Yanga, Andrew Vincent 'Dante'
  Kiungo wa Simba, Muzamil Yassin akipasua katikati ya viungo wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi (kulia) na Pius Buswita (kushoto)
  Mshambuliaji wa Simba, Mrundi Laudit Mavugo akifumua shuti huku beki wa Yanga, Kevin Yondan akikwepa

  Katika mchezo huo, uliochezeshwa na refa Heri Sasii ambaye mara kadhaa alikuwa akilalamikiwa na wachezaji wa Yanga uwanjani kwa uchezeshaji wake, Kichuya alifunga bao lake dakika ya 57 baada ya pasi ya Erasto Nyoni aliyekutana na mpira uliopanguliwa na kipa wa Yanga, Youthe Ristand kufuatia krosi ya Emmanuel Okwi.
  Kichuya alionyeshwa kadi ya njano kwa kuchelewesha muda kwa kwenda kushangilia mbali.
  Hata hivyo, bao hilo halikudumu sana, kwani dakika tatu baadaye Yanga walisawazisha kupitia kwa Chirwa aliyemalizia krosi ya winga Geoffrey Mwashiuya aliyepokea pasi ya Ibrahim Ajib.
  Sasii pia aliwaonyesha kadi za njano wachezaji wa Yanga beki Juma Abdul dakika ya 70 na mshambuliaji, Ibrahim Ajib dakika ya 69 wote kwa kupingana na maamuzi yake.

  Pamoja na sare hiyo, Yanga ndiyo waliotengeneza nafasi zaidi dhidi ya wapinzani wao, lakini umaliziaji wao mbaya uliwanyima japo bao la kuongoza.
  Lakini ni Simba ndiyo walioanza kulitia misukosuko lango la Yanga dakika ya 22, baada ya mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi kuunganishia nje krosi nzuri ya beki wa kulia, Erasto Nyoni.
  Yanga wakajibu dakika ya 23 baada ya kiungo Mkongo, Papy Kabamba Tshishimbi kufumua shuti kali lililokwenda nje sentimita chache baada ya kuukuta mpira uliotemwa na kipa Aishi Manula wa Simba kufuatia shuti la Mwashiuya.
  Tshitshimbi tena dakika ya 30 akafumua shuti kali baada ya kuukuta mpira uliookolewa na mabeki wa Simba kufuatia shuti la mpira wa adhabu la beki Juma Abdul.
  Dakika ya 31 Chirwa aliondoka vizuri na mpira kutokea katikati ya Uwanja hadi nje kidogo ya boksi na kufumua shuti lililokwenda juu ya lango la Simba hadi upande wa pili.
  Kipindi cha pili, timu zote zilionekana kuja na mbinu mpya katika kusaka mabao, safari hii Yanga ndiyo walioanza kuwashitua Simba baada ya Mwashiuya kufumua shuti kali dakika ya  55 ambalo liliokolewa na Manula.
  Baada ya mabao mfululizo Kichuya akianza dakika ya 57 na Chirwa akifuatia dakika ya 60, timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa zamu, ingawa tahadhari iliongezeka.
  Beki Mganda, Juuko Murshid alijitwisha vizuri kona ya kiungo Mnyarwanda Haruna Niyonzima kujaribu kuifungia Simba bao la pili dakika ya 66, lakini mpira ukaenda juu ya lango la Yanga.
  Yanga wakajibu dakika ya 68 baada ya Ajib kufumua shuti kali kufuatia pasi ya Tshtishimbi, lakini mpira ukaenda nje.
  Winga Emmanuel Martin aliyetokea benchi kipindi cha pili aliikosesha Yanga bao la ushindi dakika ya 71 baada ya kupiga shuti dhaifu lililodakwa na kipa Manula kufuatia krosi ya Chirwa.
  Yanga wakapandishia shambulizi lingine mwishoni mwa dakika hiyo, lakini Ajib tena akapiga shuti ambalo liliokolewa ns mshambuliaji wa Simba, John Bocco aliyetokea benchi.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Youthe Rostand, Juma Abdul, Gadiel Michael, Andrew Vincent ‘Dante’, Kelvin Yondani, Papy Kabamba Tshitshimbi, Pius Buswita, Raphael Daudi/Pato Ngonyani dk65, Obrey Chirwa, Ibrahim Ajib na Geoffrey Mwashiuya.
  Simba SC; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid, Method Mwanjali, James Kotei/Jonas Mkude dk75, Shiza Kichuya, Muzamil Yassin/Said Ndemla dk84, Emmanuel Okwi, Laudit Mavugo/John Bocco dk75 na Haruna Niyonzima. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA YAIVIMBIA SIMBA, SARE 1-1 MABAO YA KICHUYA NA CHIRWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top