• HABARI MPYA

    Thursday, October 26, 2017

    MBEYA CITY WAPANIA KUIZIMA AZAM PALE PALE CHAMAZI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MBEYA City wameweka kambi hosteli za Jeshi la Wokovu, eneo la Kurasini, Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wao wa kesho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Azam FC.
    Meneja wa MCC, Geoffrey Katepa ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo mjini Dar es Salaam kwamba wapo hapa tangu juzi na wamekuwa wakifanya mazoezi yao Uwanja wa Uhuru.
    “Leo tumefanya mazoezi yetu ya mwisho hapa Uwanja wa Uhuru kujiandaa na mchezo wetu wa kesho dhidi ya wenyeji wetu, Azam, dhamira kuu ikiwa ni kutopoteza tena mechi,”amesema.
    Katepa amesema anafahamu mchezo huo utakuwa mgumu kwa sababu Azam watakuwa wanacheza nyumbani kwao, lakini watapigana kiume kuhakikisha wanawazima hapo hapo Azam Complex.
    “Niseme tu kwamba tunawaheshimu wapinzani wetu, ni timu nzuri na ina wachezaji wazuri na walimu wazuri. Lakini hata sisi tuna wachezaji wazuri na walimu wazuri na pia ni timu nzuri na ndio maana tupo kwenye nafasi nzuri katika msimamo wa Ligi Kuu,”.
    “Tunajua kabisa mchezo utakuwa mgumu, ila sisi tunaomba marefa wachezeshe kwa haki ili mshindi apatikane kutokana na matokeo ya uwanjani na si ujanja ujanja mwingine,”amesema kiungo huyo wa zamani wa Yanga.   
    Mbeya City inashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 11 baada ya kucheza mechi saba, ikizidiwa pointi moja na Singida United iliyo nafasi ya tano na inazidiwa pointi mbili na Azam FC iliyo nafasi ya nne.
    Simba, Yanga na Mtibwa Sugar zote zinafungana kileleni mwa Ligi Kuu kwa kila timu kuwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi sana pia.
    Mechi nyingine za Ligi Kuu zinatarajiwa kuchezwa Jumamosi, mabingwa watetezi, Yanga watamenyana na Simba, Uwanja wa Uhuru, Maji Maji wataikaribisha Mwadui FC Uwanja wa Maji Maji mjini Songea, Mtibwa Sugar wataikaribisha Singida United Uwanja wa Manungu, Turiani mjini Morogoro, Lipuli watakuwa wenyeji wa Mbao FC Uwanja wa Samora mjini Iringa na Kagera Sugar wataikaribisha Ndanda FC Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MBEYA CITY WAPANIA KUIZIMA AZAM PALE PALE CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top