• HABARI MPYA

  Jumamosi, Oktoba 28, 2017

  MECHI YA WATANI AMBAYO SIMBA INAPEWA NAFASI KUBWA YA KUIFUNGA YANGA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  LEO ndiyo Oktoba 28 iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu na sasa tunasubiri Saa 10:00 jioni iwadie ili refa Heri Sasii apulize kipyenga kuanzisha mchezo wa mahasimu wa jadi, Simba na Yanga Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
  Ni mwendelezo wa mbio za ubingwa wa Ligi Kuu, lakini ndani yake kuna vita ya upinzani wa jadi baina ya timu hizo, safari hii Yanga wakiingia kinyonge kuwavaa Simba watakaoibuka vifua mbele.
  Simba wanajivunia hali nzuri ya kiuchumi kwa sasa, wakitoka kwenye kambi nzuri zaidi, kwanza hoteli ya Mtoni Marine, Zanzibar na baadaye Serena mjini Dar es Salaam, huku wachezaji wake wakiahidiwa zawadi nzuri mno wakishinda leo.
  Yanga wameamua kushikamana pamoja na hali ngumu inayowakabili, waliweka kambi mjini Morogoro na jana wamelala hoteli ya Protea ambako watatokea kuingia Uwanja wa Uhuru jioni leo kwenda kuwaonyesha Simba wao ni mabingwa wa soka Tanzania haijalishi wapo katika hali gani.
  Hii ilikuwa Agosti 23, Simba wakishinda kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0 mechi ya Ngao

  Kiufundi Simba wanaonekana kuwa vizuri zaidi ya Yanga msimu huu, wakiwa na kikosi kipana chenye wachezaji wa viwango vya juu karibu kila idara ukilinganisha na mahasimu wao.
  Kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog amekuwa hana shida kupanga kikosi hata inapotokea mmoja kati ya wachezaji aliokuwa anawapa nafasi amepata dharula, kwani ana wachezaji wengi wazuri.
  Kutokana na beki Salim Mbonde kuwa majeruhi, katika mchezo uliopita wakishinda 4-0 dhidi ya Njombe, Omog alimpanga beki mpya aliyesajiliwa kutoka Toto Africans, Yussuf Mlipili na akacheza vizuri beki ya kati, ingawa wengi walijua angepangwa Mganda, Juuko Murshid.     
  Yanga pamoja na kukabiliwa na majeruhi wengi kati ya wachezaji wake tegemeo wa kikosi cha kwanza, lakini pia wachezaji wake wapya iliyowasajili bado hawajaonyesha uwezo uliotarajiwa, ukiondoa Ibrahim Ajib, Gardiel Michael na Papy Kabamba Tshishimbi. 
  Pamoja na hayo, kocha Mzambia, George Lwandamina amekuwa akitumia weledi na uzoefu wake kuhakikisha anabadilisha mifumo mara kwa mara kulingana na aina ya wachezaji anaoingia nao kwenye mchezo.
  Baada ya muda mrefu wa kucheza na mshambuliaji mmoja, mechi mbili zilizopita Lwandamina ameanza kutumia washambuliaji wawili Ajib na Mzambia Obrey Chirwa aliyekosekana mechi za mwanzoni mwa msimu kutokana na kuwa majeruhi.
  Na ndiyo kipindi hicho timu imevuna mabao mengi zaidi, imeshinda mabao sita kwenye mechi mbili kuelekea mchezo wa leo.
  Gumzo kubwa kuelekea mchezo wa leo ni washambuliaji Emmanuel Okwi upande wa Simba, na Ajib upande wa Yanga, kutokana na hao kuwa vinara wa mabao timu zao kwa sasa.
  Ajib atakuwa akicheza mechi ya pili tangu aondoke Simba kuja kwa mahasimu, baada ya Agosti 23 kuwepo kikosini Yanga ikifungwa kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0 kwenye mechi ya Ngao ya Jamii.
  Okwi amerudi Simba Julai, lakini ni mzoefu wa mechi za watani tangu mwaka 2010 na amewahi kucheza Yanga pia kwa nusu msimu mwaka 2014.
  Lakini wote Simba na Yanga wana wachezaji wengine ambao wanaweza wakaifanya siku ya leo iwe yao, mfano Shiza Kichuya, Laudit Mavugo, Haruna Niyonzima, Muzamil Yassin au yeyote upande wa Wekundu wa Msimbazi na Chirwa, Geoffrey Mwashiuya, Papy Kabamba Tshishimbi, Raphael Daudi hata Pius Buswita upande wa Yanga.
  Uzoefu wa mechi kubwa hususan za watani wa jadi, safari hii upo zaidi Simba na ndio huo unawapa kiburi zaidi viongozi, wapenzi na wanachama wa klabu hiyo kuelekea mchezo wa leo. 
  Lakini pia Simba haijafungwa na Yanga tangu Februari 20, mwaka 2016 ilipochapwa 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu, mabao ya Donald Ngoma dakika ya 39 na Amissi Tambwe dakika ya 72.
  Baada ya hapo, mechi nne zilizofuata Wekundu wa Msimbazi walishinda tatu na kutoka sare mara moja.
  Oktoba 1, mwaka walitoa sare ya 1-1, Amissi Tambwe akianza kuifungia Yanga dakika ya 26, kabla ya Shiza Kichuya kuisawazishia Simba dakika ya 87, kabla ya Januari 10, mwaka huu Wekundu wa Msimbazi kushinda tena kwa penalti 4-2 baada ya sare ya 0-0 kwenye Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi Uwanja wa Amaan, Zanzibar.  
  Februari 26, Simba wakatoka nyuma kwa bao la penalti la Simon Msuva dakika ya tano na kushinda tena Simba 2-1 kwa mabao ya Mrundi Laudit Mavugo dakika ya 66 na Kichuya dakika ya 81, kabla ya Agosti 23, mwaka huu kushinda tena kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0 kwenye mechi ya Ngao ya Jamii.
  Vipi leo, ni Simba tena, au Yanga atafuta unyonge? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona. Dakika 90 zitatoa majibu. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MECHI YA WATANI AMBAYO SIMBA INAPEWA NAFASI KUBWA YA KUIFUNGA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top