• HABARI MPYA

  Jumatano, Oktoba 25, 2017

  YANGA WAWEKA KAMBI MOROGORO

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  YANGA waliingia kambini rasmi jana mjini Morogoro kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Simba Jumamosi Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
  Kikosi kiliwasili majira ya Saa 12:00 jioni kwa basi lake, kikitokea Shinyanga na moja kwa moja kuingia kambini kabla ya leo asubuhi kufanya mazoezi ya kwanza.
  Hata hivyo, tofauti na mahasimu wao, Simba wameweka wazi kwamba kambi yao ipo Zanzibar, Yanga wao wanaonekana kufanya siri.
  Msemaji wa Yanga, Dissmas Ten jana alisema kwamba kwamba timu ingerejea Dar es Salaama jana na baada ya hapo ndipo ingekwenda kambini.
  Yanga iliondoka Shinyanga Saa 10:00 Alfajiri jana baada ya mapumziko siku moja kufuatia ushindi wa 4-0 katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu dhidi ya wenyeji, Stand United Jumapili.
  Na taarifa zinasema wachezaji waliobaki Dar es Salaam kiungo Thabani Kamusoko na washambuliaji, Mzimbabwe mwenzake, Donald Ngoma na Mrundi Amissi Tambwe wameondoka mapema leo kwenda kuungana na wenzao kambini Moro.
  Nyasi bandia za Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam zinatarajiwa kutimbika kwa mchezo wa watani wa jadi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumamosi kuanzia Saa 10:00 jioni.
  Watatu hao hawakusafiri na timu wiki iliyopita kwa mechi za Kanda ya Ziwa kutokana na kuwa majeruhi na sasa wanarudi kikosini kuongeza nguvu baada ya kupona.
  Pamoja na kuwakosa wachezaji wake hao nyota watatu kwa muda mrefu, lakini imemudu kwenda sawa na mahasimu wao, Simba katika mbio za ubingwa.
  Simba, Yanga pamoja na Mtibwa Sugar zote zinalingana kwa pointi hivi sasa, kila moja ikiwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi saba na mshindi wa Jumamosi atatanua kwapa kileleni, wakati sare inaweza kuwashusha wote, iwapo Wakata Miwa wa Manungu watashinda dhidi ya Singida United Jumapili.    
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA WAWEKA KAMBI MOROGORO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top