• HABARI MPYA

  Jumatano, Oktoba 25, 2017

  KIPA WA ZAMANI WA CDA, SIGARA RASHID MAHADHI AFARIKI DUNIA

  Na Salma Suleiman, DAR ES SALAAM
  GOLIKIPA wa zamani wa timu za CDA ya Dodoma na Sigara ya Dar es Salaam, Rashid Omar Mahadhi amefariki dunia usiku wa kuamkia leo mjini Dar es Salaam akiwa ana umri wa miaka 43.
  Mdogo wa marehemu, Waziri Omar Mahadhi, mchezaji wa zamani wa Coastal Union, Yanga na Moro United, ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba Rashid alifariki Saa 7.00 usiku wa jana baada ya kufikishwa tu hospitali ya Rufaa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
  Waziri alisema Rashid aliamka mzima wa afya jana na akaenda kwenye shughuli zake kama kawaida na jioni alikwenda kwenye timu yake ya Abajalo, ambayo yeye ni kocha wa makipa kwa ajili ya mchezo wa Ligi Daraja la Pili Tanzania Bara dhidi ya Changanyikeni.
  Rashid Omar Mahadhi amefariki dunia usiku wa jana akiwa ana umri wa miaka 43

  Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Tandika Mabatini, Abajalo ilifungwa mabao 3-0 na Waziri amesema baada ya bao la tatu ndipo hali ya kaka yake ilibadilika na kuanza kuwa mbaya kwa mujibu Kocha Mkuu wa Abajalo, Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ ambaye anajitolea kuifundisha timu hiyo ya mtaani kwake. 
  “Walirudi naye nyumbani vizuri tu baada ya mechi, lakini bado hali yake haikuwa nzuri. Kufika kama kwenye saa tano usiku hali yake ikazidi kuwa mbaya, ikabidi wamkimbize hospitali ya Palestina. Mimi nilikuwa nyumbani kwangu, Kimara Bonyokwa nikapigiwa simu na Mzee Kibadeni ndipo nikaenda Palestina. Kufika pale hali ya kaka ikawa imezidi kuwa mbaya, ikabidi tumkimbize Muhimbili, ambako tulipofika tu mapokezi wakati tunaandikisha akafariki dunia,”amesema Waziri.
  Kiungo huyo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, amesema msiba wa Rashid aliyewika miaka ya 1990 katika Ligi Kuu ya Bara, upo nyumbani kwake, Kimara Bonyokwa na mwili wa marehemu utasafirishwa mapema kesho kwa mazishi kwenye makaburi ya Mnyangani, Tanga.
  Waziri amesema marehemu ambaye alipatwa na ugonjwa wa kiharusi kwa zaidi ya mwaka sasa, ameacha mke, Jazira na mtoto, Mahadhi mwenye umri wa miaka 18 sasa. Mungu aipumzishe kwa amani roho ya marehemu. Amin.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KIPA WA ZAMANI WA CDA, SIGARA RASHID MAHADHI AFARIKI DUNIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top