• HABARI MPYA

  Jumapili, Oktoba 29, 2017

  TANZANIA BARA YANG'ARA MBIO ZA KILOMITA 10 KMKM ZANZIBAR

  Na Salum Vuai, ZANZIBAR
  USHINDI wa kwanza kwa upande wa wanawake na wanaume kwenye mbio za kilomita 10 katika mashindano yaliyoandaliwa na Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM), zote zimechukuliwa na wakimbiaji kutoka Tanzania Bara.
  Katika michuano hiyo iliyofanyika leo ikianzia makao makuu ya KMKM Kibweni mnamo saa 1:10 asubuhi,  na kumalizikia viwanja vya Maisara mjini Zanzibar, Dickson Marwa kutoka Musoma aliibuka wa kwanza upande wa wanaume baada ya kukimbia kwa dakika  29:52:02.
  Nafasi ya pili ilikwenda kwa Mkenya Lameck Mwakio aliyetimka kwa dakika 29:52:07, akifuatiwa na Nelson Mbuya aliyepeperusha bendera ya Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar (JKU), ambaye pumzi zake zilimuwezesha kukimbia kwa dakika 29:59:07.
  Washiriki wa mbio  za kilomita 10 zinazoandaliwa na KMKM wakikimbiza kupitia mitaa mbali mbali ya Zanzibar 
  Mshindi wa kwanza kwa upande wa wanawake Sara Ramadhani Makera kutoka Arusha akimaliza mbio hizo kwa kutumia dakika 37:18.25,  
  Mshindi wa kwanza wa mbio za kilomita 10 mwaka 2017 Dickson Marwa kutoka Dar es Salam akimaliza mbio hizo katika viwanja vya Maisara kwa kutumia dakika 29:52.02

  Kwa matokeo hayo washindi hao walizawadiwa medali za dhahabu, fedha na shaba mtawalia.
  Mwanadada Sarah Ramadhan kutoka Arusha alifanikiwa kunyakua medali ya dhahabu baada ya kuwatupa wafukuza upepo wenzake kwa dakika 37:18:25, huku Sharo Myryuti (Kenya) akishika nafasi ya pili akikimbia kwa dakika 37:38:43 na kuondoka na medali ya fedha.
  Mwanariadha mzoefu wa michuano ya kimataifa Zakia Mohammed Mrisho kutoka Arusha, aliambulia namba tatu akifikisha muda wa dakika 38:43:45 na kutia mikononi medali ya shaba.
  Mbali na mfukuzano huo mkuu, pia mashindano hayo yalipambwa kwa mbio za kushajiisha, ambapo mwanariadha mstaafu Faida Salmin kutoka Mkwajuni aliibuka kidedea kwa upande wa wazee wanawake kwenye kilomita mbili, huku Othman Aziz wa Jang’ombe akiwafunika wazee wenzake kwa upande wa wanaume.
  Aidha resi kwa wakimbiaji wenye ulemavu wanawake, ziliwashuhudia wasichana kutoka Amani waking’ara kwa kushika nafasi zote tatu za kwanza, ambao kwa mpangilio ni Hadaa Khatib Simai, Amina Daud na Fatma Said.
  Wakimbiaji wenye ulemavu wanaume, mshindi wa kwanza alikuwa Wahid Abdalla Abdalla (Jang’ombe), akifuatiwa na Ali Bora Msheza na Khamis Ali (wote kutoka Mkwajuni).
  Wengine wenye ulemavu walioshinda kwenye patashika hizo ni Shukuru Khalfan (Dar es Salaam), Haji Ali Haji (Amani) pamoja na Yaina Hussein (Mwembeladu) ambao waliungana na washindi wengine kupokea zawadi mbalimbali walizokabidhiwa na viongozi tafauti akiwemo mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ayoub Mohammed Mahmoud.
  Halikadhalika kulikuwa na michuano ya kuvuta kamba pamoja  na kufukuza kuku iliyoshirikisha wachezaji wanawake na wanaume.
  Michuano hiyo ya tatu kuandaliwa na KMKM, mbali na mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Mjini Ayoub Mohammed Mahmoud, pia ilihudhuriwa na Waziri wa Habari, Utalii, Utalii na Michezo Rashid Ali Juma pamoja na Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake  na Watoto Moudline Castico.
  Viongozi wengine ni Mshauri wa Rais Michezo na Utamaduni Chimbeni Kheri, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Sadalla ‘Mabodi’, Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) Amour Hamil Bakari, Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania Filbert Bayi, makamanda wa vikosi mbalimbali vya ulinzi na usalama na wadau wengine wa michezo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TANZANIA BARA YANG'ARA MBIO ZA KILOMITA 10 KMKM ZANZIBAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top