• HABARI MPYA

  Jumatano, Oktoba 25, 2017

  SAMATTA AMALIZA UKAME WA MABAO WA MIEZI MIWILI, AFUNGA DAKIKA YA MWISHO GENK YASHINDA 2-0

  Na Mwandishi Wetu, GENK
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania Mbwana Ally Samatta usiku huu amemaliza ukame wa mabao wa mechi tisa, baada ya kuifungia klabu yake, KRC Genk bao la pili ikishinda 2-0 dhidi ya Club Brugge katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji, Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
  Katika mchezo wa leo, Samatta alifunga dakika ya 90 akimalizia pasi ya Clinton Mata, baada ya Ruslan Malinovskiy kuanza kuifungia timu hiyo bao la kwanza dakika ya 43.
  Kabla ya leo, mara ya mwisho Samatta aliifungia mabao mawili Genk Agosti 13, mwaka huu ikishinda 5-3 dhidi ya wenyeji, Royal Antwerp FC katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Bosuilstadion, Deurne na baada ya hapo akacheza mechi tisa bila kufunga kabla ya kumaliza ukame dakika ya mwisho leo.
  Mbwana Samatta (katikati) usiku huu amemaliza ukame wa mabao wa miezi miwili leo 

  Na hilo linakuwa bao la 22 kwake katika mechi 68 za mashindano yote tangu alipowasili Genk Januari mwaka jana akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Katika mechi hizo, Samatta ambaye ni mshindi wa tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika mwaka jana alipokuwa na Mazembe, 40 ameanza na mechi 24 ametokea benchi.
  Kikosi cha KRC Genk kilikuwa: Vukovic, Uronen, Colley, Aidoo, Mata, Berge/Heynen dk18, Malinovskyi, Writers, Pozuelo/Brabec dk82, Samatta na Ingvartsen/Buffel dk90+2.
  Club Brugge : Horvath, Wesley/Dennis dk45, Day, Limbombe, Vanaken, Cools/Fossils dk71, Denswil, Vormer, Nakamba/Refaelov dk83, Decarli na Mechele.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA AMALIZA UKAME WA MABAO WA MIEZI MIWILI, AFUNGA DAKIKA YA MWISHO GENK YASHINDA 2-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top