• HABARI MPYA

  Jumatatu, Oktoba 30, 2017

  MBEYA CITY WATAKA KUMALIZIA HASIRA ZAO KWA SIMBA

  Na David Nyembe, MBEYA
  TIMU ya Mbeya City imewataarifu Simba SC, kwamba waende Mbeya wakijua wafungwa katika mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Baada ya sare ya 1-1 na mabingwa watetezi, Yanga SC Jumamosi Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Simba wanatarajiwa kuwa wageni wa Mbeya City Jumapili Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
  Na akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo mjini hapa, Meneja wa Mbeya City, Geoffrey Katepa amesema kwamba baada ya kupoteza mchezo wa ugenini dhidi ya Azam FC, hasira zao watamalizia kwa Simba.
  “Tumefungwa 1-0 na Azam pale Dar es Salaam jambo ambalo ni kinyume na malengo yetu, sisi hatutaki kupoteza mechi, kwa hiyo lazima mchezo wetu unaofuata tushinde ili tujipoze machungu,”amesema.
  Katepa amesema wanaiheshimu Simba ni timu nzuri na ina wachezaji wazuri, lakini hata Mbeya City wapo vizuri na kwa kudhihirisha hilo wanataka kushinda Jumapili.
  “Simba ni timu nzuri, tumewaona hadi Jumamosi walipocheza na Yanga, lakini wanafungika na sisi hapa tutawafunga lazima,”amesema.
  Mbeya City inashika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zake 11 ilizovuna kwenye mechi nane, ikizidiwa pointi moja na jirani zao, Lipuli walio nafasi ya sita.
  Simba SC inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 16 sawa na Yanga, Azam FC na Mtibwa Sugar. 
  Ligi Kuu itaendelea Ijumaa, Maji Maji FC wakiikaribisha Stand United Uwanja wa Maji Maji mjini Songea, wakati Jumamosi Singida watakuwa wenyeji wa Yanga Uwanja wa Namfua, Singida na Ndanda FC wataikaribisha Mtibwa Sugar Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
  Mechi nyingine za Jumamosi, Kagera Sugar wataikaribisha Tanzania Prisons Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Njombe Mji FC wataikaribisha Mbao FC Uwanja wa Saba Saba na Azam FC watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Jumapili kutakuwa na mechi mbili, mbali na Mbeya City kuwa wenyeji wa Simba, Lipuli FC nao wataikaribisha Mwadui FC Uwanja wa Samora mjini Iringa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MBEYA CITY WATAKA KUMALIZIA HASIRA ZAO KWA SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top