• HABARI MPYA

  Ijumaa, Oktoba 27, 2017

  SIMBA WAREJEA DAR KWA NDEGE MAALUM KUIVAA YANGA KESHO

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KIKOSI cha Simba kimerejea asubuhi ya leo mjini Dar es Salaam kwa ndege maalum ya kukodi kutoka kisiwani Zanzibar, ambako waliweka kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga kesho.  
  Simba wameteremkea Uwanja wa ndege wa zamani, maarufu kama Terminal One na moja kwa moja kuelekea katikati ya Jiji, ambako wataweka kambi katika hoteli ya Serena, tayari kwa mchezo wa kesho Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  Wachezaji wa Simba walioonekana watulivu mno wakati wanawasili Terminal One, walikuwa wakitoka ndani na moja kwa moja kupanda basi la timu lililokuwa hapo linawasubiri, huku kukiwa na ulinzi mkali wa ‘makomandoo’ wa timu.
  Wachezaji wa Simba wakiongozwa na kiungo Muzamil Yassin wakati wanawasili Uwanja wa Ndege wa zamani leo asubuhi mjini Dar es Salaam
  Haruna Niyonzima (katikati) wakati anawasili na Simba Uwanja wa Ndege wa zamani leo asubuhi 
  Basi la wachezaji wa Simba likiwa Uwanja wa Ndege wa zamani leo asubuhi

  Simba iliweka kambi katika hoteli ya bora zaidi kwa sasa nchini, Mtoni Marine yenye nyota saba tangu Jumatatu huku wakiwa wakifanya mazoezi Uwanja wa Amaan katika kuhakikisha wanaendeleza ubabe wao kwa watani.
  Simba haijafungwa na Yanga tangu Februari 20, mwaka 2016 ilipochapwa 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu, mabao ya Donald Ngoma dakika ya 39 na Amissi Tambwe dakika ya 72.
  Baada ya hapo, mechi nne zilizofuata Wekundu wa Msimbazi walishinda tatu na kutoka sare mara moja.
  Oktoba 1, mwaka walitoa sare ya 1-1, Amissi Tambwe akianza kuifungia Yanga dakika ya 26, kabla ya Shiza Kichuya kuisawazishia Simba dakika ya 87, kabla ya Januari 10, mwaka huu Wekundu wa Msimbazi kushinda tena kwa penalti 4-2 baada ya sare ya 0-0 kwenye Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi Uwanja wa Amaan, Zanzibar.  
  Februari 26, Simba wakatoka nyuma kwa bao la penalti la Simon Msuva dakika ya tano na kushinda tena Simba 2-1 kwa mabao ya Mrundi Laudit Mavugo dakika ya 66 na Kichuya dakika ya 81, kabla ya Agosti 23, mwaka huu kushinda tena kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0 kwenye mechi ya Ngao ya Jamii.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA WAREJEA DAR KWA NDEGE MAALUM KUIVAA YANGA KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top