• HABARI MPYA

  Jumatano, Oktoba 25, 2017

  WENGER ‘AWASHANGAA’ CHELSEA KWA KUMFUKUZA NKETIAH

  KOCHA Arsene Wenger amesema hakujua kwa nini Chelsea ilimuondoa Eddie Nketiah katika akademi yao, baada ya kinda huyo wa umri wa miaka 18 kufunga mabao mawili katika mechi yake ya kwanza Arsenal jana.
  Mzaliwa huyo wa London, Nketiah alitokea benchi dakika ya 85 na kuisawazishia Arsenal dhidi ya Norwich City kwenye Kombe la Carabao, kabla ya kufunga la ushindi katika dakika za nyongeza.
  Lakini shujaa huyo wa sasa timu ya vijana ya Arsenal, alikuwa kwenye akademi ya Chelsea hadi alipofikisha umri wa miaka 14 alipobadili njia London na kwenda Emirates baada ya kuachwa Stamford Bridge.
  Eddie Nketiah alifukuzwa Chelsea kabla ya kuokolewa na Arsenal ambako ameanza kung'ara sasa PICHA ZAIDI GONGA HAPA

  Wenger, akiwa amemshuhudia mchezaji wa kwanza aliyezaliwa baada ya yeye kuwa kocha wa Arsenal Septemba mwaka 1996 kuifungia The Gunners, amesema hajui sababu zilizowafanya Chelsea wamuache Nketiah aondoke.
  “Sijui nini kilitokea Chelsea,” amesema Mfaransa huyo. “Amefunga mabao katika timu ya vijana, sijui kwa nini wamemuacha aondoke,” alisema.
  “Sijui kwa nini. Unaona hiyo zaidi na zaidi. Vijana wadogo wanaondoka kutoka klabu moja hadi nyingine. Sijui,”.
  Nketiah alikuwa akitumika kama kiungo Chelsea, lakini akahamia nafasi ya ushambuliaji baada ya kujiunga na Arsenal, ambayo ilimpa nafasi ya kucheza mechi yake ya kwanza dhidi ya BATE Borisov kwenye michuano ya Europa League na jana usiku Kombe la Carabao.
  “Ana ubora wa kiwango cha juu, na ni mmoja wa wachezaji waliokuwa nami kwenye maandalizi ya msimu mpya na nilijua atafanya nini,”alisema Wenger. “Lazina nitasema nimevutiwa, nafikiri alikuwa hata hajazaliwa wakati nimekwishafika hapa. Lakini ni vizuri. Maisha yanatoa nafasi kwa vijana wadogo na ni matumaini yangu atakuwa na maisha marefu Arsenal. Tunajivunia kuwapa nafasi vijana wadogo,”.
  Arsenal ilimnasa Nketiah mwaka 2015, ilipomkaribisha kufanya mazoezi siku mbili tu baada ya kuachwa na Chelsea, waliomsitishia ofa ya kumsomesha shule pia. 
  “Siku Arsenal walipoonyesha wana nia na mimi, ilikuwa ni moja ya siku za furaha kwangu naweza kukumbuka,” alisema Nketiah wakati huo.
  “Haikuwa tu kwa sababu nilikuwa shabiki wa Arsenal, lakini siku mbili kabla niliambiwa ningeachwa na Chelsea na nisingepewa tena nafasi ya kuendelea kusomeshwa shule msimu huu. Nilifadhaika mno, lakini Arsenal wakanitafuta, waliwasiliana na familia yangu na kunikaribisha kwa mazoezi. Ndani ya wiki, niliambiwa kwamba ningeendelea kusomeshwa shule. Nafikiri ni muhimu kuibuka haraka baada ya kuanguka na Arsenal wamenipa nafasi ya kufanya hivyo,”amesema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: WENGER ‘AWASHANGAA’ CHELSEA KWA KUMFUKUZA NKETIAH Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top