• HABARI MPYA

  Ijumaa, Oktoba 27, 2017

  YANGA SC WAREJEA LEO DAR TAYARI KUIVAA SIMBA KESHO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA SC wanaondoka mchana wa leo Morogoro baada ya mazoezi ya asubuhi kurejea Dar es Salaam tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Simba SC kesho Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  Na wakifika Dar es Salaam, watakwenda kuweka kambi nyingine katika hoteli moja nzuri katikati ya Jiji, ambako ndiko wataondokea kesho kwenda Uwanja wa Uhuru kwa ajili ya mchezo huo utakaoanza Saa 10:00 jioni.
  Yanga ilikuwa Morogoro tangu Jumanne jioni ikitokea Shinyanga, ambako Jumapili walishinda 4-0 dhidi ya wenyeji Stand United katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
  Wachezaji wa Yanga wakati wanatoka Shinyanga kuingia Morogoro kwa kambi yao fupi

  Baada ya mazoezi ya siku tatu, mabingwa hao watetezi wanarejea Dar es Salaam kujaribu kusaka ushindi wa kwanza dhidi ya Simba baada ya mechi nne za mashindano yote tangu msimu uliopita.
  Mara ya mwisho Yanga kuvuna ushindi kwa Simba ilikuwa ni Februari 20, mwaka 2016 wakishinda 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu, mabao ya Donald Ngoma dakika ya 39 na Amissi Tambwe dakika ya 72.
  Baada ya hapo, mechi nne zilizofuata, Yanga wakafungwa tatu, moja ya Ligi Kuu na nyingine za Kombe la Mapinduzi na Ngao ya Jamii.
  Oktoba 1, mwaka walitoa sare ya 1-1, Amissi Tambwe akianza kuifungia Yanga dakika ya 26, kabla ya Shiza Kichuya kuisawazishia Simba dakika ya 87, kabla ya Januari 10, mwaka huu Wekundu wa Msimbazi kushinda tena kwa penalti 4-2 baada ya sare ya 0-0 kwenye Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi Uwanja wa Amaan, Zanzibar.  
  Februari 26, Simba wakatoka nyuma kwa bao la penalti la Simon Msuva dakika ya tano na kushinda tena Simba 2-1 kwa mabao ya Mrundi Laudit Mavugo dakika ya 66 na Kichuya dakika ya 81, kabla ya Agosti 23, mwaka huu kushinda tena kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0 kwenye mechi ya Ngao ya Jamii.
  Na kesho Yanga watatafuta ushindi wa kwanza dhidi ya Simba ndani ya mechi tano.
  Jarida la Yanga ukurasa wa mbele unavyoonekana 

  Wakati huo huo: Yanga imezindua jarida lake la kila mwezi ambalo litakuwa na mkusanyiko wa habari na makala maalum kuhusu klabu hiyo.
  Kwa mujibu wa Msemaji wa Yanga, Dismass Ten, jarida hilo litaana kuuzwa leo. “Yanga Magazine’, itaanza kuuzwa rasmi leo kuanzia saa 3:00 Asubuhi Makao Makuu ya Klabu (Jangwani) na kesho Uwanja wa Uhuru. Kwa Morogoro linapatikana kwa Hamad Islam, kwa wale wanaohitaji kuwa mawakala, wanakaribishwa. Kwa maelezo zaidi wasiliana na Idara ya Habari – 0757569752,”amesema Ten.
   Kurasa za ndani za jarida la Yanga 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC WAREJEA LEO DAR TAYARI KUIVAA SIMBA KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top