• HABARI MPYA

  Jumatano, Oktoba 25, 2017

  BOCCO YUKO FITI KUICHEZEA SIMBA DHIDI YA YANGA JUMAMOSI, KESI YA AKINA AVEVA YAAHIRISHWA TENA

  Na Salum Vuai, ZANZIBAR
  MSHAMBULIAJI wa Simba, John Raphael Bocco yuko fiti kwa mchezo na mahasimu wa jadi, Yanga Jumamosi Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam baada ya kupona maumivu ya mguu.
  Mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, jana na leo amefanya mazoezi kikamilifu katika kambi ya Zanzibar kujiandaa na mechi ya Jumamosi dhidi ya Yanga.
  Pamoja na Bocco, mchezaji mwingine aliyekuwa majeruhi, kiungo Mohammed ‘Mo’ Ibrahim naye yuko fiti na anaendelea na mazoezi Zanzibar.
  Katika kambi hiyo, Simba inawakosa kipa Said Mohammed ‘Ndunda’, mabeki Shomary Kapombe na Salim Mbonde ambao wote ni majeruhi wa muda mrefu.
  John Bocco (kushoto) akijifua na wachezaji wenzake Uwanja wa Amaan, Zanzibar leo
  Wachezaji wa Simba wakiendelea na mazoezi leo Zanzibar

  Kapombe hajacheza kabisa tangu arejee Simba kutoka Azam FC kutokana na kuumia kwenye michuano ya Kombe la COSAFA nchini Afrika Kusini akiwa na timu ya taifa, Taifa Stars Julai mwaka huu.
  Ndunda aliuami Agosti kwenye kambi ya mazoezi Zanzibar kujiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga uliochezwa Agosti 23, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakati Mbonde aliumia kwenye mechi dhidi ya timu yake ya zamani, Mtibwa Sugar Oktoba 15 Uwanja wa Uhuru.
  Mbonde ambaye atakuwa nje hadi katkati ya Novemba, aliumia siku moja na Bocco, ambaye yeye alipewa mapumziko ya wiki moja tu, wakati Ndunda na Kapombe hawatarajiwi kabisa kucheza mwaka huu. 
  Wakati huo huo: Kesi ya utakatishaji fedha inayowakabili viongozi wakuu wa klabu ya Simba, Rais Evanve Aveva na Makamu wake, Geoffrey Nyange 'Kaburu' imeahirishwa tena hadi Novemba 6, mwaka huu kwa sababu jalada la uchunguzi wake bado lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
  Hayo yamebainishwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Vitalis Peter aliyemueleza Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Kisutu mjini Dar es Salaam, Victoria Nongwa na akaomba kesi hiyo ipangiwe tarehe nginyine.
  Baada ya kuelezwa hayo, Wakili wa washitakiwa, Evodius Mtawala alidai upande wa mashtaka ulitoa taarifa kama hiyo September 18, mwaka huu na tangu siku hiyo ni zimepita siku 37, hivyo ameiomba Mahakama iwahimize ofisi ya DPP kulifuatilia jalada hilo, kwa sababu wateja wake wapo ndani na maisha yao yamekuwa ni kama yamesimama.
  Akijibu hoja hizo za Wakili Mtawala, Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa TAKUKURU, Leonard Swai alidai kuwa ni kweli na kwamba wanajitahidi kulifuatilia lakini hadi sasa bado halijatoka kwa DPP.
  Hata hivyo, Swai alidai kuwa  sheria haijampa muda DPP wa kukaa na jalada ila kwa upande wao ni kuhimiza tu. Hakimu Nongwa baada ya kusikiliza hoja hizo, aliwataka upande wa Mashtaka walifuatilie na kuliwasilisha hadi katika tarehe hiyo iliyopangwa tena.
  Ikumbukwe, Aveva na Kaburu wanakabiliwa na mashitaka matano yakiwemo ya utakatishaji fedha, ambayo hayana dhamana na wote wapo rumande gereza la Keko tangu Juni 29.
  Miongoni mwa mashitaka yanayowakabili ni pamoja na kughushi nyaraka zinazodaiwa kuwa klabu ya Simba inawalipa madeni watuhumiwa hao kiasi cha dola za Kimarekani 300,000 (Zaidi ya shilingi milioni 700 za kitanzania).
  Makosa mengine ni Aveva kutoa nyaraka za uongo kwa Benki ya CRDB Tawi la Azikiwe Dar es Salaam Machi 10, 2016, la tatu ni kutakatisha fedha kinyume cha sheria, ambapo inadaiwa rais huyo na Kaburu walikula njama za kufanya uhalifu huo.
  Shitaka la nne ni Kaburu kutakatisha fedha dola 300,000 na kuziweka katika Benki ya  Barclays Tawi la Mikocheni mjini Dar es Salaam, na la tano ni kutakatisha fedha  likimhusu tena, Makamu wa Rais, Kaburu anayedaiwa kumsadia Aveva kutakatisha fedha katika benki ya Barclays baada ya kughushi nyaraka.

  Kwa sasa nafasi zao zinakaimiwa na Salim Abdallah ‘Try Again’ katika Urais na Iddi Kajuna katika Makamu wa Rais, ambao wamejitahidi kuiongoza vizuri klabu tangu wenzao wapate matatizo hayo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: BOCCO YUKO FITI KUICHEZEA SIMBA DHIDI YA YANGA JUMAMOSI, KESI YA AKINA AVEVA YAAHIRISHWA TENA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top