• HABARI MPYA

  Alhamisi, Oktoba 26, 2017

  KONE AITOA KWA MAMA YAKE TUZO YA 'UUNGWANA' YA FIFA

  MSHAMBULIAJI wa Togo, Francis Kone ameitoa kwa mama yake, Akoudji Tuzo ya Mchezo wa Kiungwana ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) aliyoshinda Jumatatu.
  Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 alipewa tuzo hiyo baada ya kumsaidia mchezaji wa timu pinzani, Martin Berkovec asiumeze ulimi wake wakati wa mechi ya Ligi ya Czech mapema mwaka huu.
  “Nampenda sana mama yangu na hii tuzo ni mali yake,” amesema Kone, ambaye wakati huo alikuwa anachezea Slovacko wakati huo. “Ni zawadi kubwa niliyopewa katika maisha yangu,”.
  “Namshukuru mama yangu na familia yangu – ambao wanasherehekea – na watu hao wanaonisapoti kwa ninachokifanya,”.
  Kone hakuhudhuria tuzo hizo Jumatatu usiku mjini London, lakini atakabidhiwa tuzo yake kesho wakati wakala wake aliyempokelea tuzo hiyo atakapowasili Jijini Brno, Czech.
  Tangu kutangazwa mshindi wa tuzo hiyo, Kone – ambaye alihama Slovacko kujiunga na wapinzani wa Ligi Kuu ya Czech, Zbrojovka Brno mwezi Julai – amesema amekuwa akipokea ujumbe wa kupongezwa kwa wingi na kutakiwa kila la heri.
  “Napokea simu kutoka kwa kila mmoja kila sehemu kunitumia pongezi,” alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Togo ambaye alicheza mechi mbili mwaka 2013.
  Februari mwaka huu, mshambuliaji huyo alipongezwa kwa kuokoa maisha ya Berkovec baada ya kipa wa Bohemians 1905 alipokaribia kuumeza ulimi wake kufuatia kugongana na mchezaji mwenzake na kuanguka na kupoteza fahamu.
  Kone, alitumia vidole vyake kuuvuta ulimi wa Berkovec kumzuia kuumeza baada ya kugongana na mchezaji mwenzake, Daniel Krch.
  Berkovec alimshukuru sana Kone baada ya tukio hilo; “Ningependa kumshukuru Francis Kone kwa kuniokoa na dharula,” aliandika Berkovec baadaye kwenye ukurasa wake wa Facebook. “Nashukuru nimepata nafuu, na asante tena!!!”
  “Siwezi kusimama hapa, kumuangalia mtu anaangamia, bila ya kufanya chochote,” Kone alisema mwezi Aprili.
  Mzaliwa huyo wa Ivory Coast ambaye alichezea Togo kutokana na familia yake, Kone alisema amewahi kukutana na matukio ya aina hiyo matatu kabla.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KONE AITOA KWA MAMA YAKE TUZO YA 'UUNGWANA' YA FIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top