• HABARI MPYA

  Alhamisi, Oktoba 26, 2017

  HERI SASII KWA MARA YA PILI MFULULIZO KUCHEZESHA SIMBA NA YANGA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  REFA bora wa msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Elly Sasii ndiye atakayechezesha mchezo wa mahasimu wa jadi, Simba na Yanga Jumamosi Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
  Hii itakuwa mara ya pili mfululizo kwa Sasii kupuliza kipyenga katika mechi ya mahasimu hao, baada ya Agosti 23, mwaka huu kutekeleza pia jukumu hilo kwenye mechi ya Ngao ya Jamii, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Simba ikishinda kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0.
  Elly Sasii ndiye atakayechezesha mchezo wa Simba na Yanga Jumamosi Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam

  Sasii ni refa chipukizi, ambaye amekwishaanza kupata uzoefu wa kimataifa kwa kuchezesha mechi za kimataifa pia, kwani ndiye aliyekuwa refa wa mchezo wa kufuzu Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zinazohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee, kati ya Uganda na Sudan Kusini Julai mwaka huu.
  Alichezesha pia mechi ya kirafiki kati ya Everton ya England na Gor Mahia ya Kenya kabla ya Septemba 3, mwaka huu kuchezesha mchezo kati ya wenyeji Taifa Stars na Botswana.
  Kuelekea mchezo huo, Simba wameweka kambi kwenye hoteli ya Mtoni Marine visiwani Zanzibar wakati Yanga ipo mjini Morogoro.
  Timu hizo zinakutana kila timu ikiwa imevuna pointi 15 hadi sasa katika Ligi Kuu, sawa na Mtibwa Sugar ya Morogoro baada ya kucheza mechi saba. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HERI SASII KWA MARA YA PILI MFULULIZO KUCHEZESHA SIMBA NA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top