• HABARI MPYA

  Jumapili, Oktoba 29, 2017

  TFF WAMEFANIKIWA KUWAZUIA WATU KWENDA KWA WINGI UWANJANI JANA

  WAMAELFU ya wapenzi wa soka Dar es Salaam jana waliamua kubaki nyumbani kushuhudia mchezo wa mahasimu wa jadi, Simba na Yanga kupitia Televisheni.
  Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baina ya Simba na Yanga iliyomalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1, inaweza kuwa ya kwanza baada ya muda mrefu sana kuhudhuriwa na watu wachache.
  Wastani wa watu 15,000 tu ndiyo waliingia uwanjani jana, jambo ambalo halikutarajiwa kabisa na si picha nzuri kwa soka ya Tanzania.
  Wengi tunafahamu kwamba soka ya nchi hii imebaki inabebwa na upinzani wa Simba na Yanga, hivyo inapotokea watu wanaanza kupuuza na mechi hiyo, hizo ni dalili mbaya
  kwa soka yetu.
  Tunapaswa kushituka na kujiuliza kwa kufanya tathmini ya kina na ya kitaalamu, isiyo ya dhana wala juu juu ili kujua kwa nini hakukuwa na watazamaji wengi uwanjani jana.
  Mambo kadhaa yanatajwa kwa sasa kama sababu, kwamba watu walitishwa na vyombo vya Habari kwamba Uwanja wa Uhuru ni mdogo kutakuwa vurumai ya kugombea kuingia, hivyo wakaona wabaki nyumbani.
  Septemba 9, mwaka huu Simba ilikwenda kwenye Uwanja mdogo zaidi wa Azam Complex, Chamazi na mbali pia, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam kumenyana na wenyeji, Azam FC na watu walikwenda kwa wingi, waliokosa nafasi wakaondoka.
  Hii ni maana yake hoja ya udogo wa Uwanja katika burudani ya soka haiwezi kuwa sababu hapa, hivyo tunapaswa kuzama ndani zaidi na kutafuta kiini cha tatizo.
  Wengine wanasema mchezo huo kuonyeshwa kwenye Televisheni imesababisha watu kutokwenda kwa wingi Uwanja wa Uhuru. Je, hii ni Simba na Yanga kuonyeshwa mbashara kwenye Televisheni?
  Jibu ni hapana, kwa zaidi ya miaka mitano sasa mechi zote za Simba na Yanga zimekuwa zikionyeshwa kwenye Televisheni na watu wanakwenda kwa wingi uwanjani, tena kwenye Uwanja mkubwa wa Taifa.     
  Nikirudia kuasa, haya mambo si ya kupuuzwa kwa vingozi wenye dhamira njema na soka ya nchi hii, ambayo imebaki inapumulia Usimba na Uyanga, nashauri uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ulifanyie kazi na kuishia kumaliza tatizo kwa dhana au hisia.
  Watazame ndani na nje ya Uwanja ni mambo yapi ambayo ni kero kwa watu wanaokwenda uwanjani – mfano ulinzi na usalama wa raia na mali zao, wepesi na urahisi wa watu kupafikia uwanjani na dhana ya starehe wanayoifuata, je wanavipata?
  Watu wanatoka maeneo tofauti ya Jiji wengine mbali mno, mbele ya Mbezi zote, za barabara ya Morogoro na Bagamoyo, Chamazi, Mwasonga, Geza Ulole, Mwandege, Chanika na wengine mikoa jirani ya Pwani, Tanga, Zanzibar na Morogoro kuja kushuhudia mechi hizo.
  Pamoja na kero ya foleni ya kupafikia Uwanja wa Uhuru au Taifa, lakini wanapofika wanakutana na kero nyingine ndogo ndogo, ambazo ni kubwa mfano vizuizi vya kuwazuia kusogea hadi uwanjani na magari yao.
  Kuna magari huwa yanawekwa kuziba njia eneo la Chuo Kikuu cha Ualimu Dar es Salaam (DUCE) na upande wa pili kutokea barabara ya Mandela, nako askari wa usalama barabarani huweka vizuizi na kuruhusu gari maalum tu.
  Hii ni adhabu kubwa linapokuja suala la starehe na katika wakati kama huu ambao mechi zinaonyeshwa mbashara kwenye Televisheni, watu wanaamua kuepukana na adha hizo kwa kwenda kuangalia mpira kwenye TV.
  Lakini pia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama navyo, vimekuwa na njia moja tu rahisi ya kupambana na vurugu zinapotokea, ambayo ni kupiga bunduki za gesi za sumu hata kwenye vurumai ndogo, jambo ambalo husababisha athari kwa watu wengi hata wasio na hatia.
  Wakati mwingine watu wasio na hatia wamekuwa wakipigwa na askari ama bila kosa, au kwa makosa madogo tu yanayohitaji kuelimishwa tu.
  Ubabe na lugha zisizofaa kwenye mageti ya kuingilia uwanjani shida pia. Mpangilio mbovu wa uingiaji na mfumo ambao bado unalalamikiwa wa Kielektroniki kwamba una mlolongo mrefu na usio wa uhakika wakati mwingine tatizo pia. Kuna wakati mambo husimama kwa sababu ya eti mtandao mbovu, ni kero isiyovumilika.
  Pamoja na hayo, ukirejea kwenye mchezo wa jana, maeneo ambayo hayakuwa na watu wengi ni mzunguko ambako kiingilio kilikuwa Sh. 10,000, zaidi ya nusu ya kiingilio kilichozoeleka kwenye eneo hilo katika mechi za Simba na Yanga. Hilo limetazamwa?
  Hali halisi ya maisha Tanzania kwa sasa haiwapi nafasi Watanzania wengi kutumia fedha nyingi kwa anasa – mambo ya watu weledi hufikiriwa kwanza kabla ya kufanyiwa maamuzi, aliyeamua kiingilio cha Sh. 10,000 mzunguko alifikiria nini?
  Na kama lengo tuseme ilikuwa ni kufanya kiingilio kikubwa katika eneo la mzunguko ili watu wasiende kwa wingi kwa sababu Uwanja ni mdogo, basi tuseme TFF wamefanikiwa. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TFF WAMEFANIKIWA KUWAZUIA WATU KWENDA KWA WINGI UWANJANI JANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top