• HABARI MPYA

  Jumanne, Oktoba 31, 2017

  SINGIDA UNITED WAKATAA UNDUGU NA YANGA, WASEMA JUMAMOSI ACHA ‘KICHAFUKE’ NAMFUA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  UONGOZI wa Singida United umesema kwamba uhusiano wao na Yanga ni wa kawaida na hautaingilia matokeo ya mchezo wao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumamosi Uwanja wa Namfua, Singida.
  Kwa mara ya kwanza Jumamosi wiki hii, Singida United watacheza Uwanja wa nyumbani, Namfua baada ya mechi zake zote za awali za nyumbani kucheza mkoa jirani, Dodoma katika Uwanja wa Jamhuri.
  Na kuelekea mchezo huo, Mkurugenzi wa Singida United, Sanga Festo amesema kwamba wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanashinda dhidi ya mabingwa watetezi, Yanga.
  Benchi la Ufundi la Singida United linaongozwa na kocha wa zamani wa Yanga, Mholanzi, Hans van der Pluijm
  “Kwanza nataka niondoe hofu iliyopo juu ya urafiki wetu na Yanga, sisi hatuna urafiki na Yanga, Yanga ni washiriki wenzetu wa Ligi Kuu na Jumamosi tunakutana nao kuwania ushindi ili tujiweke kwenye nafasi nzuri katika msimamo,”amesema.
  Pamoja na hayo, Sanga amesema ni kweli kuna baadhi ya viongozi wakuu wa timu hiyo, akiwemo mlezi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alikuwa mpenzi wa Yanga, lakini kwa sasa amebaki kuwa Sindida tu.
  “Tangu amekuwa mlezi wa Singida, Mheshimiwa Mwigulu amejivua kabisa upenzi wa Yanga na sasa hivi hata akienda kuwaangalia wakicheza, anakwenda kama mpenzi wa kawaida,”amesema.  
  Uwanja wa Namfua upo tayari kwa mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu baada ya muda mrefu 

  Festo amesema kwamba Uwanja wa Namfua upo tayari kwa mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu baada ya muda mrefu kufuatia kufanyiwa ukaguzi na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
  Amesema kikosi kinatarajiwa kuanza mazoezi jioni ya leo Uwanja wa Namfua, baada ya kurejea kutoka Manungu, mkoani Morogoro ambako Jumapili walitoka sare ya 0-0 na wenyeji, Mtibwa Sugar.
  Festo amesema katika mchezo huo watamkosa mchezaji mmoja tu, beki Mzimbabwe, Elisha Muroiwa ambaye ni majeruhi. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SINGIDA UNITED WAKATAA UNDUGU NA YANGA, WASEMA JUMAMOSI ACHA ‘KICHAFUKE’ NAMFUA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top