• HABARI MPYA

  Jumanne, Oktoba 31, 2017

  SIMBA WAMSHUTUMU REFA SASII KUWABEBA YANGA...WADAI ALIWANYIMA PENALTI MBILI ZA HALALI

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Simbe imelalamika kunyimwa penalti mbili na refa Heri Sasii katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga SC uliomalizika kwa sare ya 1-1 Jumamosi Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya klabu, Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Hajji Sunday Manara amesema refa alikwenda na matokeo yake uwanjani. 
  Manara aliwawekea Waandishi wa Habari video ya mchezo huo kuwaonyesha namna ambavyo refa Sasii hakutoa penalti licha ya mpira kuwagonga mikononi beki, Kevin Yondan na kiungo Mkongo, Papy Kabamba Tshishimbi Jumamosi.
  Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi (kushoto) akizungumza na refa Heri Sasii (kulia) Jumamosi
  Manara aliyewabeza watani wao hao wa jadi, kwamba ni kawaida yao kupendelewa na marefa kila wanapokutana na Simba amesema watapeleka malalamiko Bodi ya Ligi dhidi ya refa huyo na wengine walioionea timu yao katika mechi zilizotangulia.
  Akasema huo ni mwendelezo wa matukio ya klabu yake kutotendewa haki na marefa katika mechi za Ligi Kuu msimu huu, akidai walinyimwa pia penalti mbili katika mechi dhidi ya Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, kabla ya wapinzani wao wengine, Singida United kupewa penalti ya utata Uwanja wa CCM Kambarage Shinyanga.
  Simba ilitoa sare ya 2-2 na Mbao FC kabla ya kushinda 3-1 dhidi ya Stand United, katika mchezo ambao pia walikataliwa bao zuri la mshambuliaji wao, Laudit Mavugo.
  Pamoja na hayo, Manara amelalamikia kitendo cha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kukataa ombi la klabu, Simba na Yanga kutaka mchezo wao ufanyike Uwanja mkubwa wa Taifa na kuupeleka Uwanja mdogo wa Uhuru.
  Manara amesema hali hiyo ilizikosesha klabu fedha kutokana na watazamaji kutojitokeza kwa wingi kwa kuhofia usalama wao kutokana na udogo wa Uwanja wa Uhuru. 
  Aidha, Manara mtoto wa mchezaji wa zamani wa Yanga, Sunday Manara ‘Kompyuta’ amesema kwamba kikosi cha Simba sasa kinaelekeza nguvu zake katika mchezo wake ujao dhidi ya Mbeya City Jumapili Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
  Amesema kwamba kikosi kitaondoka Jijini Ijumaa kwenda Mbeya, ambako kitakaa kwa muda mrefu kutokana na kukabiliwa na mechi nyingine pia za Ligi Kuu Nyanda za Juu Kusini. Amesema hakuna majeruhi mpya kikosini, ukiondoka kipa Said Mohammed ‘Nduda’ na mabeki Shomary Kapombe na Salim Mbonde.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA WAMSHUTUMU REFA SASII KUWABEBA YANGA...WADAI ALIWANYIMA PENALTI MBILI ZA HALALI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top