• HABARI MPYA

    Saturday, April 11, 2015

    KLUIVERT AWANYANYASA TANZANIA ELEVEN, APIKA BAO, APIGA BAO, BARCA YASHINDA 2-1

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    MAGWIJI wa Tanzania wamefungwa mabao 2-1 na magwiji wa Barcelona katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni ya leo.
    Wakiongozwa na mkali wa mabao zamani Uholanzi, Patrick Kluivert, Barcelona walikuwa wa kwanza kupata bao dakika tisa, Luis Garcia kwa kichwa.
    Sifa zimuendee Kluivert aliyechonga kona maridadi ikaunganishwa nyavuni na Garcia.
    Awali ya hapo, beki wa zamani wa Simba SC, Mustapha Hoza alifanya kazi nzuri baada ya kuokoa mpira uliokuwa unaelekea nyavuni, kufuatia Mingo kumpiga chenga kipa wa Tanzania, Manyika Peter dakika ya tano.

    Patrick Kluvert akiwa amembeba mtoto albino, Sharifa kabla ya mchezo huo leo Uwanja wa Taifa

    Tanzania ilijibu shambulizi hilo dakika moja baadaye, baada ya kiungo wa zamani wa Yanga na Simba, Yussuph Macho ‘Musso’ kupiga shuti kali lililodakwa na Barca, Tito.
    Kluivert alikaribia kufunga dakika ya 21 kama si shuti lake kali kutoka nje sentimita chache na dakika ya 32, Macho alipiga shuti zuri lililokwenda nje kidogo ya lango.
    Hatimaye jitihada za Tanzania zilizaa matunda dakika ya 44, baada ya kupata bao la kusawazisha lililofungwa na Macho kwa shuti maridadi. 
    Kipindi cha pili, Tanzania walianza na mabadiliko wakimpumzisha kipa Manyika Peter na nafasi yake kuchukuliwa na Juma Kaseja, beki John Mwansasu akampisha Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’.
    Mabadiliko hayo hayakuizuia Barca kupata bao la ushindi dakika ya 86, mfungaji Kluivert kwa penalti baada ya Mustapha Hoza kumuangusha Kluivert mwenyewe kwenye boksi.
    Refa Keneth Mapunda alimuonyesha kadi za njano mara mbili Hoza dakika ya 60 na 86 baada ya kumchezea rafu Kulvert mara zote.

    Mshambuliaji wa Barcelona, Luis Carreras akimtoka beki wa Tanzania, Mustapha Hoza leo Uwanja wa Taifa

    Pamoja na ushindi huo, Barcelona iliyoonekana kuwa na wachezaji walioacha mpira siku za karibuni zaidi, ilizidiwa umiliki wa mpira na Tanzania ambayo ilitumia wachezaji waliostaafu muda mrefu, ukiondoa Juma Kaseja na Haruna Moshi ‘Boban’.
    Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Peter Manyika/Juma Kaseja dk46, Shadrack Nsajigwa, Abubakar Kombo John Mwansasu/Bakari Malima dk46, Mustapha Hoza, Shaaban Ramadhan/Nico Nyagawa dk21, Nassor Mwinyi Bwanga/Deo Lucas dk31, Haruna Moshi ‘Boban’, Yussuph Macho/Salvatory Edward dk50, Bita John na Duwa Said. 
    Barcelona; Tito Bonayo, Mandieta, Mingo, Alber Thomas, Roger Garcia, Luis Milla, Luis Carreras, Santi Ezquerro, Patrick Kluivert, Luis Garcia na Simao Sabrosa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KLUIVERT AWANYANYASA TANZANIA ELEVEN, APIKA BAO, APIGA BAO, BARCA YASHINDA 2-1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top