• HABARI MPYA

    Wednesday, June 03, 2026

    NI SENEGAL MABINGWA WA AFCON U17, SERENGETI BOYS YAFA KWA MATUTA


    TIMU ya Senegal imefanikiwa kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17(AFCON U17) baada ya ushindi wa penalti 4-2 dhidi ya Tanzania kufuatia sare ya kufungana bao 1-1 usiku huu Uwanja wa Moulay El Hassan Jijini Rabat nchini Morocco.
    Kiungo Hamisi Chenga Mihambo alianza kuifungia Serengeti Boys dakika ya saba, kabla ya mshambuliaji Ibrahima Dione kuwasawazishia Young Lions of Teranga dakika ya 64, dakika mbili tu baada ya kuingia kuchukua nafasi ya Cheikh Omar Sy.
    Katika mikwaju ya penalti leo haikuwa siku nzuri kwa chipukizi wa Kitanzania, mabeki Idrisa Kasim Kilendemo akipiga juu na Hussein Ally Mbegu yake ikiokolewa na kipa 
    Serigne Diouf anayefahamika zaidi kwa jina la Assane Sarr.
    Waliofunga penalti za Simba Wadogo wa Teranga ni Souleymane Commissaire Faye, Émile Niaga Sadio, Ibrahima Dione na Cheikh Thior huku za Serengeti Boys zikifungwa na Elick Shaban Yusuph na Razaki Juma Mbegelend pekee.
    Pamoja na kukosa Kombe, huu umekuwa mwaka mzuri kw Tanzania katika ushiriki wake wa michuano ya U17 ya wavulana kihistoria, ikiweka rekodi ya kufika Fainali baada ya kuvuka hatua ya makundi kwa mara ya kwanza sambamba na kufuzu Kombe la Dunia.  
    Mafanikio hayo yanakuja Tanzania ikishiriki kwa kwa mara ya tatu AFCON U17 baada ya mwaka 2017 nchini Gabon na 2019 nyumbani, Tanzania ambako mara zote walitolewa katika hatua ya makundi. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NI SENEGAL MABINGWA WA AFCON U17, SERENGETI BOYS YAFA KWA MATUTA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top