• HABARI MPYA

    Saturday, October 26, 2019

    MECHI ZA NDANDA FC ZAAHIRISHWA BAADA YA TIMU KUPATA AJALI TABORA JANA IKIWA SAFARINI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MECHI mbili za Ligi Kuu ya Tanzania Bara za Ndanda FC dhidi ya wenyeji Kagera Sugar iliyokuwa ifanyike kesho Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na dhidi ya Biashara United iliyopangwa kuchezwa Jumatano zimeahirishwa.
    Taarifa ya Bodi ya Ligi iliyosainiwa na Mtendaji wake Mkuu, Boniphace Wambura imesema kwamba sababu za kuuahirisha michezo hiyo ni klabu ya Ndanda kupata ajali jana.
    Basi la timu ya Ndanda FC lilipata ajali jana wilayani Nzega mkoani Tabora likiwa safarini kuelekea mkoani Kagera na wachezaji watano, Aziz Sibo, Paul Maona, Hemed Khoja, Nassor Saleh na Omar Ramadhan waliripotiwa kupata maumivu madogo madodo.
    Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Barnabas Mwakalukwa alisema jana kwamba ajali hiyo imetokea baada ya gari ya Ndanda kuligonga basi la abiria la Mtei na kusababisha majeraha kwa wachezaji watano wa Ndanda.
    Mechi za kesho Ligi Kuu zitaendelea kama kawaida kesho ambazo ni Ruvu Shooting na Azam FC Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Biashara United na Namungo FC Uwanja wa Karume mjini Musoma na Lipuli FC na Coastal Union Uwanja wa Samora mjini Iringa.
    Aidha, Mwadui FC watakuwa wenyeji wa JKT Tanzania Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga na Singida United watawakaribisha mabingwa watetezi, Simba SC Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha. 
    Jumatatu kutakuwa na mechi mbili mjini Mwanza, Uwanja wa Nyamagana Alliance FC dhidi ya Tanzania Prisons na CCM Kirumba ni Mbao FC dhidi ya Mbeya City.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MECHI ZA NDANDA FC ZAAHIRISHWA BAADA YA TIMU KUPATA AJALI TABORA JANA IKIWA SAFARINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top