• HABARI MPYA

  Jumamosi, Oktoba 19, 2019

  MTIBWA SUGAR YAPATA USHINDI WA KWANZA LIGI KUU BARA, YAICHAPA NDANDA FC 1-0 MTWARA

  Na Mwandishi Wetu, MTWARA 
  TIMU ya Mtibwa Sugar imepata ushindi wa kwanza katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu baada ya kuwachapa wenyeji, Ndanda FC 1-0 jioni ya leo Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
  Sasa Mtibwa Sugar, mabingwa wa Ligi Kuu misimu miwili mfululizo 1999 na 2000 wanafikisha pointi tano baada ya kucheza mechi sita, nyingine tano wakifungwa tatu na kutoa sare mbili.
  Bao pekee la Mtibwa Sugar leo limefungwa na beki wake wa kati Dickson Daud Mbekya dakika ya 35, akimalizia pasi ya beki wa kulia, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’. 
  Mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Riphat Khamisi akimpongeza Dickson Daudi baada ya kufunga bao pekee leo

  Ndanda FC walipoteza nafasi ya kusawazisha bao hilo baada ya Omary Ramadhan kukosa penalti dakika ya 66.
  Mtibwa Sugar iliuanza msimu vibaya kutokana na kumkosa kocha wake, Zubery Katwila aliyekuwa na timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, ambayo aliiwezesha kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) Challenge U20 nchini Uganda.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Namungo FC imetumia vyema Uwanja wa nyumbani, Majaliwa huko Ruangwa mkoani Lindi kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Lipuli FC bao pekee la Hashim Manyanya dakika ya 76, akimalizia pasi ya Jukumu Kibanda.
  Nayo Mbao FC imelazimishwa sare ya 1-1 na Ruvu Shooting Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.  Fully Maganga alianza kuifungia Ruvu Shooting dakika ya 20, kabla ya Jordan John kuisawazishia Mbao FC dakika ya 50.
  Nayo Tanzania Prisons ikalazimishwa sare ya 1-1 na Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya. Ismail Azizi alianza kuifungia Tanzania Prisons dakika ya 60, kabla ya Nassor Kapama kuisawazishia Kagera Sugar dakika ya 78.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MTIBWA SUGAR YAPATA USHINDI WA KWANZA LIGI KUU BARA, YAICHAPA NDANDA FC 1-0 MTWARA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top