• HABARI MPYA

  Thursday, October 24, 2019

  MO DEWJI AWAZAWADIA WACHEZAJI SIMBA SC PIKIPIKI, SIMU NA ‘RICE COOKER’ KWA KUFANYA VIZURI MSIMU ULIOPITA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu ya Simba SC, Mohammed ‘Mo’ Dewji leo amemkabidhi kila mchezaji wa klabu hiyo pikipiki, mashine ya kupikia wali kijulikanacho kama rice cooker na simu ya mkononi.
  Zoezi hilo limefanyika leo mjini Dar es Salaam kwenye ofisi za Mohamed Enteprises Limited (MeTL), ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Mo Dewji kufuatia timu kufanikiwa kutetea taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanania Bara na kufika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita. 
  Pamoja na hayo, Mo Dewji amemteua aliyekuwa Afisa Mtendaji Mkuu, Crescentius Magori kuwa Mshauri Binafsi wa Mwenyekiti wa Bodi.
  Magori atakuwa na jukumu la kumshauri mwenyekiti mambo mbalimbali ambayo yatasaidia kuboresha utendaji ambao utawezesha klabu kupata mafanikio zaidi.
  Magori ana uzoefu mkubwa, kwani mbali na kuwa Mtendaji Mkuu wa Simba pia amewahi kuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mjumbe Kamati ya CAF ya Soka la Ufukweni na Futsal, Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Baraza la vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
  “Uteuzi wake umeanza jana Jumatano Oktoba 23, 2019. Kwa niaba ya Wanasimba, tunamtakia kila la kheri kwenye majukumu yake mapya tukiamini kwamba atatoa msaada mzuri kwa klabu ambao utatuwezesha kupiga hatua kubwa na hasa kutokana na uzoefu wake mkubwa kwenye soka,”imesema taarifa ya Mo Dewji.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MO DEWJI AWAZAWADIA WACHEZAJI SIMBA SC PIKIPIKI, SIMU NA ‘RICE COOKER’ KWA KUFANYA VIZURI MSIMU ULIOPITA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top