• HABARI MPYA

    Friday, October 11, 2019

    MENEJA WA RHINO RANGERS NA WACHEZAJI WAWILI WATIWA HATIANI KWA KUMPIGA REFA GEITA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MENEJA wa klabu ya Rhino Rangers, Ali Rhumba amepelekwa Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) baada ya kumpiga Mwamuzi Msaidizi, Omari Mataka na kumjeruhi chini ya jicho katika mechi dhidi ya Geita Gold FC Septemba 21 Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita.
    Hatua hiyo imechukuliwa katika kikao cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kilichofanyika Oktoba 7, mwaka huu kupitia mwenendo na matukio mbalimbali ya ligi hiyo.
    Katika mechi hiyo namba 10 B, wachezaji wa Rhino Rangers Simon Joseph Kiula aliyevalia jezi namba 5 na Julius Elias Masunga jezi namba 26, nao wanapelekwa Kamati ya Nidhamu kwa kuwarushia mawe waamuzi baada ya kumalizika mechi hiyo.
     
    Polisi waliokuwa uwanjani walijitahidi kupambana na licha ya kupata upinzani kutoka kwa wanajeshi kadhaa waliombatana na Rhino Rangers.
    Mechi namba 8A: Boma FC 2 v Majimaji 0- Meneja wa timu ya Majimaji, Shaibu Ibrahim amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa kutolewa katika benchi kwa kadi nyekundu baada ya kumtukana Mwamuzi katika mechi hiyo iliyochezwa Septemba 22, 2019 Uwanja wa Mwakangale uliopo Kyela, Mbeya. 
    Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42(20) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti kwa Viongozi.
    Mechi namba 10A: Dodoma FC 1 v Friends Rangers 0- Wachezaji Ahmed Abbas Iddy (Friends Rangers) na Mbwana Bakari (Dodoma FC) wamefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kila mmoja baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kupigana katika mchezo huo uliofanyika Septemba 21, 2019 Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. 
    Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 38(3) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
    Mechi namba 1B: Gwambina FC 3 v Arusha FC 0- Klabu ya Arusha imepewa Onyo kutokana na timu yake kuchelewa kuingia uwanjani kwa dakika 19. 
    Timu hiyo iliingia saa 9:19 badala ya saa 9:00 katika mechi hiyo iliyochezwa Septemba 14, 2019 kwenye Uwanja wa Gwambina mkoani Mwanza.
    Vilevile Arusha FC imepewa Onyo Kali kutokana na wachezaji wake kuingia uwanja kwa kuruka uzio wa ndani badala ya kutumia mlango walioelekezwa. 
    Adhabu zote hizo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.
    Mechi namba 2B: Geita Gold FC 2 v Mashujaa FC 2- Klabu ya Geita imepewa Onyo kutokana na timu yake kuchelewa kuingia uwanjani kwa dakika 20. 
    Timu hiyo iliingia saa 9:20 badala ya saa 9:00 katika mechi hiyo iliyochezwa Septemba 14, 2019 kwenye Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita. 
    Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.
    Kocha Msaidizi wa Mashujaa FC, Kajembe Abdallah amefungiwa mechi tatu na kutozwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) kwa kutolewa katika benchi kwa kadi nyekundu baada ya kumtukana Mwamuzi Msaidizi. 
    Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41(11) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Udhibiti kwa Makocha.
    Mechi namba 9B: Gwambina FC 1 v Stand United 0– Kamishna Nestory Matiku amepewa Onyo kwa kutoa taarifa isiyojitosheleza ya mechi hiyo iliyochezwa Septemba 21, 2019 katika Uwanja wa Gwambina mkoani Mwanza.
    Mechi namba 12B: Sahare All Stars 1 v Green Warriors 1- Kipa wa Green Warriors, Shabani Dihile amepewa Onyo Kali kwa kutoa shutuma dhidi ya waamuzi kuwa walichezesha kwa maelekezo ya viongozi mechi hiyo iliyochezwa Septemba 22, 2019 katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. 
    Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.
    Mechi namba 13B: Stand United 3 v Green Warriors 2- Klabu ya Green Warriors imetozwa faini y ash. 200,000 (laki mbili) baada ya wachezaji wake kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi katika mchezo huo uliofanyika Septemba 27, 2019 Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. 
    Adhabu ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Daraja la Kwanza kuhusu Taratibu za Mchezo.
    Mechi namba 17B: Pamba SC 1 v Geita Gold FC 2- Meneja wa Pamba SC, Jafari Juma amepelekwa Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) baada kwa kumpiga ngumi Mwamuzi, tukio lililosababisha askari polisi wamweke chini ya ulinzi katika mechi hiyo iliyofanyika Septemba 28, 2019 kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MENEJA WA RHINO RANGERS NA WACHEZAJI WAWILI WATIWA HATIANI KWA KUMPIGA REFA GEITA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top