• HABARI MPYA

  Friday, October 18, 2019

  KIINGILIO CHA CHINI MECHI YA YANGA SC NA PYRAMIDS FC NI SH 10,000 OKTOBA 27 MWANZA

  Na Asha Said, DAR ES SALAAM
  KIINGILIO cha chini katika mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baina ya wenyeji, Yanga SC na Pyramids FC ya Misri Oktoba 27 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza kitakuwa Sh. 10,000.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu leo Jangwani, Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Frederick Mwakalebela amesema kwamba kiingilio hicho kitahusu majukwaa ya mzunguko, wakati  VIP itakuwa Sh. 50,000 na Royal Sh. 70,000.
  Kikosi cha Yanga kitaondoka kesho mjini Dar es Salaam kwenda mkoani Mwanza kwa ajili ya mechi hiyo itakayotanguliwa na mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania dhidi Mbao FC Jumanne hapo hapo Kirumba.
  Mwakalebela amesema kikosi kitaondoka mapema kesho kikiwa na wachezaji 26, benchi la ufundi chini ya Kocha wake Mkuu Mwinyi Zahera, pamoja na viongozi wanne wa klabu.
  Mwakalebela alisema maandalizi ya mechi zote mbili yanaendelea vizuri ikiwa ni pamoja na wageni wao kuanza kufanya taratibu husika za sehemu ya kufikia kwa kuandaa Hoteli ya kufikia,  kwa kutumia ubalozi wa Misiri uliopo hapa nchini.
  Aidha Mwakalebela, alisema wachezaji David Molinga 'Falcao' na Mustafa Suleiman hawatatumika katika mchezo dhidi ya Pyramids, wataweza kutumika endapo timu itangia katika hatua ya makundi na katika michezo ya Ligi Kuu Bara wataendelea na kazi kama kawaida.
  Alisema wachezaji hao hawatweza kutumika sababu ya kukosa vibali kutoka CAF,  wachezaji hao hawajashiriki mashindano hayo sababu ya kukosa vibali.
  Aidha Mwakalebela alisema katika kuelekea mchezo huo uongozi wa Yanga umetoa basi maalum litakalopeleka mashabiki mkoani humo, hivyo kwa anayetaka anatakiwa kufika makao makuu ya klabu hiyo Mtaa wa Twiga, Jangwa Dar es Salaam kuonana na Kaimu Katibu Mkuu Dismas Ten.
  Alisema katika mchezo wa mpira wa miguu ni jambo nzuri kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi Uwanja ili wachezaji waweze kupata hamasa zaidi ya kimchezo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KIINGILIO CHA CHINI MECHI YA YANGA SC NA PYRAMIDS FC NI SH 10,000 OKTOBA 27 MWANZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top