• HABARI MPYA

  Jumatano, Oktoba 23, 2019

  YANGA SC YAICHAPA PAMBA 2-1 KATIKA MCHEZO WA KIRAFIKI LEO ASUBUHI CCM KIRUMBA

  Na Mwandishi Wetu, MWANZA
  TIMU ya Yanga SC imeibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Pamba SC katika mchezo wa kirafiki asubuhi ya leo Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Mchezo huo umefanyika siku moja tu baada ya Yanga SC kupata ushindi wa 1-0 dhidi ya timu nyingine ya Mwanza, Mbao FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jana jioni.
  Mabao ya Yanga SC leo yamefungwa na wachezaji wake wa kigeni watupu, Mnyarwanda Patrick ‘Papy’ Sibomana dakika ya 21 na Juma Balinya dakika ya 56, wakati la Pamba SC limefungwa na mkongwe, Shija Mkina dakika ya 26.
  Ikumbukwe jana pia bao pekee la ushindi katika mchezo dhidi ya Mbao FC limefungwa na mchezaji wa kigeni pia, Mnamibia Sadney Urikhob.

  Yanga SC ilipata pigo baada ya mshambuliaji wake Mzambia, Maybin Kalengo kukimbizwa hospitali ya Bugando kufuatia kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na kipa Metacha Mnata aliyekwenda kusimama langoni huku Ramadhani Kabwili akihamia kwenye nafasi ya ushambuliaji.
  Yanga SC ipo kambini mjini Mwanza inajiandaa na mchezo wake wa kwanza wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramids FC Jumapili wiki hii Uwanja wa CCM Kirumba. 
  Kikosi cha Yanga SC leo kilikuwa; Ramadhani Kabwili, Mustafa Suleiman, Jaffar Mohammed, Said Juma ‘Makapu’, Lamine Moro, Abdulaziz Makame, Deus Kaseke, Raphael Daudi/Gustavo Simon, Juma Balinya, Maybin Kalengo/Metacha Mnata na Patrick Sibomana. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC YAICHAPA PAMBA 2-1 KATIKA MCHEZO WA KIRAFIKI LEO ASUBUHI CCM KIRUMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top