• HABARI MPYA

    Sunday, October 20, 2019

    2019 UTAKUMBUKWA DAIMA KATIKA HISTORIA YA SOKA YA TANZANIA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    2019 unaingia kwenye orodha ya miaka ya kutosahaulika katika historia ya soka ya Tanzania baada ya Taifa Stars kukata tiketi ya kucheza Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Cameroon.
    Stars imefuzu baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya wenyeji, Sudan juzi Uwanja wa Omdurman, Mourada mjini Omdurman, shukrani kwa mshambuliaji Ditram Nchimbi aliyesababisha bao la kwanza na kufunga la pili siku hiyo.
    Kwa matokeo hayo, Taifa Stars inayofundishwa na kocha Mrundi, Etienne Ndayiragijje anayesaidiwa na wazalendo, Suleiman Matola na Juma Mgunda imefuzu CHAN ya 2020 kwa faida ya mabao ya ugenini baada ya sare ya jumla ya 2-2, kufuatia kufungwa 1-0 kwenye mchezo wa kwanza Dar es Salaam.
    Timu nyingine zilizofuzu fainali za michuano hiyo inayoshirikisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee zitakazoanza Januari 2020 ni wenyeji, Cameroon Uganda, Rwanda, Zambia, Namibia, Morocco, Zimbabwe, DRC, Kongo Tunisia, Burkina Faso, Guinea, Niger, Mali na Togo watakaoshiriki kwa mara ya kwanza.
    Nchimbi hakuwemo kikosini wakati Taifa Stars inafungwa 1-0 na Sudan kwenye mechi ya kwanza Dar es Salaam Septemba 22, lakini baada ya kuifungia mabao yote matatu klabu yake, Polisi Tanzania ikitoa sare ya ugenini ya 3-3- na vigogo, Yanga SC Oktoba 3 akaongezwa kikosini.
    Baada ya Sudan kutangulia kwa bao la Amir Kamal dakika ya 30 akimalizia krosi ya Ahmed Adam Mohamed aliyemlamba chenga beki wa kulia wa Tanzania, Salum Kimenya, Nchimbi anayecheza kwa mkopo Polisi Tanzania akawainua Watanzania kwa jitihada zake binafsi.
    Kwanza Nchimbi aliwakokota walinzi wa Sudan akiwahadaa kulia na kushoto kabla ya kuangushwa nje kidogo ya boksi na Nahodha, Erasto Edward Nyoni akaenda kufunga kwa shuti la mpira wa adhabu dakika ya 49 kuisawazishia Taifa Stars.
    Nchimbi mwenye umri wa miaka 24 akiwa anacheza mechi yake ya kwanza ya mashindano ya kimataifa na ya pili jumla baada ya ile ya kirafiki dhidi ya Rwanda mjini Kigali timu hizo zikitoka 0-0 Oktoba 14, akaifunga bao la ushindi Tanzania dakika ya 79 akimalizia pasi ya mshambuliaji mwenza Shaaban Iddi Chilunda.
    Furaha zaidi ni kwa kipa mkongwe wa Tanzania, Juma Kaseja aliyerejeshwa kikosini baada ya miaka mitano, ambaye amedaka mechi zote za kufuzu na kuipa tiketi ya CHAN nchi yake. Katika raundi ya kwanza, Tanzania iliitoa Kenya kwa penalti 4-1 baada ya sare ya jumla ya 0-0.
    Hiyo inakuwa mara ya pili kwa Taifa Stars kufuzu fainali za michuano hiyo inayoshirikisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee, baada ya mwaka 2009 nchini Ivory Coast, ikiitoa Sudan pia katika raundi ya mwisho ya kufuzu.
    Vikosi vya Taifa Stars kufuzu CHAN; dhidi ya Kenya Dar es Salaam;  Juma Kaseja, Paul Godfrey, Gardiel Michael, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Jonas Mkude, Hassan Dilunga/Kelvin John dk67, Salum Abubakar, John Bocco/Salim Aiyee dk85, Ayubu Lyanga/Ibrahim Ajibu dk54 na Idd Suleiman ‘Nado’.
    Dhidi ya Kenya Nairobi; Juma Kaseja, Paul Godfrey, Gardiel Michael, Erasto Nyoni, Kelvin Yondan, Jonas Mkude, Frank Domayo/Salim Aiyee, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco/Ayoub Lyanga, Iddi Suleiman ‘Nado’ na Hassan Dilunga/Abdulaziz Makame.
    Dhidi ya Sudan Dar es Salaam; Juma Kaseja, Gardiel Michael, Boniphace Maganga, Erasto Nyoni, Kelvin Yandani, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Shaaban Iddi Chilunda, Ayoub Lyanga/Miraji Athuman dk67, Muzamil Yassin/Hassan Dilunga dk72, Jonas Mkude na Idd Suleiman ‘Nado’.
    Dhidi ya Sudan Omdurman; Juma Kaseja, Salum Kimenya, Gardiel Michael, Erasto Nyoni, Bakari Kondo, Jonas Mkude, Miraj Athumani/Ayoub Lyanga dk64, Frank Domayo/Salum Abubakar ‘Sure Boy’ dk82, Muzamil Yassin, Ditram Nchimbi na Iddi Suleiman ‘Nado’/Shaaban Iddi Chilunda dk62.
    Ikumbukwe huu ni mwaka ambao Tanzania ilicheza tena Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zilizofanyika nchini Misri mwezi Juni, ikiwa ni mara ya pili tu kihistoria baada ya 1980, enzi hizo michuano hiyo ikijulikana kama Fainali za Kombe la Mataifa Huru ya Afrika (CAN).   
    Kwa kufuzu mfululizo fainali za michuano hii mikubwa ya Afrika – pamoja na Simba SC kufika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa, jambo lililosababisha mwaka huu nchi iingize wawakilishi wanne kwenye michuano ya klabu barani kutoka wawili, hakika 2019 unakuwa mwaka mwingine wa kukumbukwa daima katika historia ya soka ya Tanzania.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: 2019 UTAKUMBUKWA DAIMA KATIKA HISTORIA YA SOKA YA TANZANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top