• HABARI MPYA

  Jumatatu, Oktoba 28, 2019

  MBEYA CITY YAZINDUKA NA KUICHAPA MBAO FC 2-1 KIRUMBA, ALLIANCE 1-1 PRISONS NYAMAGANA

  Na Asha Said, MWANZA
  TIMU ya Mbeya City imezinduka na kupata ushindi wa ugenini wa 2-1 dhidi ya wenyeji, Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Katika mchezo wa leo uliochezeshwa na refa Martin Saanya wa Morogoro aliyesaidiwa na Sunday Kamba Abdulaziz Ally wote wa Arusha, Mbao FC ilipata pigo dakika ya kwanza tu baada ya kuanza kipindi cha pili, kufuatia mchezaji wake, Babilas Chitembe kumchezea rafu Baraka Ngusa kwenye boski.
  Rafu hiyo ilisababisha na penalti iliyowapa bao la kuongoza Mbeya City, lililofungwa na nyota wake, Peter Mapunda dakika ya 48.

  Mshambuliaji Said Khamis Junior akapoteza nafasi ya kuisawazishia Mbao FC baada ya mkwaju wake wa penalti kuokolewa na kipa Haroun Mandanda dakika ya 88 kufuatia Datus Peter kuchezewa rafu na beki wa Mbeya City, Hassan Mwasapili.
  Mshambuliaji Emmanuel Charles Lukinda akaisawazishia Mbao FC dakika ya 90 na wakati mashabiki wa timu hiyo hawajamaliza kushangilia, Peter Mapunda akaifungia Mbeya City bao la ushindi kwa shuti la mpira wa adhabu dakika ya 90 na ushei.
  Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, wenyeji Alliance FC wamelazimishwa sare ya 1-1 na Tanzania Prisons ya Mbeya Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza, Samson Mbangula akianza kuwafungia wageni dakika ya 68 kabla ya Daniel Mnayenye kuwasawazishia wenye mji wao dakika ya 75.
  Ushindi wa leo ni ahueni kwa kocha Juma Mwambusi, ambaye mchezo uliopita timu yake ilichapwa 4-1 na Kagera Sugar ya Bukoba nyumbani, Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, kwani sasa MCC inafikisha pointi saba katika mchezo wa saba na kujivuta kutoka nafasi ya 19 hadi ya 17 katika ligi ya timu 20.  
  Mbao FC inabaki na pointi zake saba baada ya kucheza mechi nane sasa ikiwa nafasi ya 16, wakati Alliance FC iliyofikisha pointi 10 katika mchezo wa saba sasa ni ya saba na Tanzania Prisons yenye pointi 11 za mechi saba ni ya tano.
  Kikosi cha Mbao FC; Abdallah Makangana, Datus Peter, Emmanuel Charles, Abdulrahman Said, Babilas Chitembe, Rajab Rashid, Jordan John, Kauswa Bernard/Haji Juma dk47, Said Junior, Adil Sultan/ Frank Paschal dk68 na Herbet Lukindo.
  Mbeya City; Haroun Mandanda, Keneth Kunambi, Hassan Mwasapili, Samson Madeleke, Ally Lundenga, Baraka Nguba, Suleiman Mangoma/Suleiman Ibrahim dk90+3, George Chota, Peter Mapunda, Gamba Iddi/Kelvin John dk60 na Notikely Masasi/Mpoki Mwakinyuke dk55.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MBEYA CITY YAZINDUKA NA KUICHAPA MBAO FC 2-1 KIRUMBA, ALLIANCE 1-1 PRISONS NYAMAGANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top