• HABARI MPYA

  Jumatano, Oktoba 23, 2019

  KALENGO NJE MIEZI MITATU BAADA YA KUUMIA KWENYE MECHI YA KIRAFIKI DHIDI YA PAMBA LEO

  Na Mwandishi Wetu, MWANZA
  MSHAMBULIAJI Mzambia wa Yanga SC, Maybin Kalengo atatakiwa kuwa nje kwa miezi isiyopungua mitatu kufuatia kuumia leo asubuhi akiichezea klabu yake mchezo wa kirafiki mazoezini Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Kalengo aliye katoka msimu wake wa kwanza baada ya kusajiliwa Julai mwaka huu kutoka ZESCO United FC ya kwao, alikimbizwa hospitali ya Bugando kufuatia kuumia kwenye mchezo huo, ambao Yanga ilishinda 2-1.
  Baada ya kukimbizwa hospitali, nafasi yake ilichukuliwa na kipa Metacha Mnata aliyekwenda kusimama langoni huku Ramadhani Kabwili akihamia kwenye nafasi ya ushambuliaji.
  Na baada ya kufanyiwa vipimo, Daktari wa Yanga SC, Shecky Mngazija akasema kwamba vipimo vinaonyesha Kalengo amepata maumivu makali na atatakiwa kupumzika kati ya wiki nane hadi 12 ili kupona. 
  Maybin Kalengo atakuwa nje kwa miezi mitatu kufuatia kuumia leo asubuhi mjini Mwanza

  Daktari wa Yanga SC, Shecky Mngazija (kushoto) akimsaidia Maybin Kalengo kutoka nje baada ya kuumia leo 

  “Mchezaji wetu ameumia leo katika mchezo wa kirafiki dhidi ya PambaFC. Taarifa za kitabibu zinaeleza kuwa majeraha yake yatachukua wiki nane hadi 12 kupona kabisa. Uongozi wa Yanga umeshafanya taratibu za kumsafirisha Kalengo kurejea Dar es Salaam kwa matibabu zaidi,”amesema Dk. Mngazija.
  Yanga SC ipo kambini mjini Mwanza inajiandaa na mchezo wake wa kwanza wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramids FC Jumapili wiki hii Uwanja wa CCM Kirumba.
  Mchezo wa leo dhidi ya Pamba umefanyika siku moja tu baada ya Yanga SC kupata ushindi wa 1-0 dhidi ya timu nyingine ya Mwanza, Mbao FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jana jioni.
  Mabao ya Yanga SC leo yamefungwa na wachezaji wake wa kigeni watupu, Mnyarwanda Patrick ‘Papy’ Sibomana dakika ya 21 na Juma Balinya dakika ya 56, wakati la Pamba SC limefungwa na mkongwe, Shija Mkina dakika ya 26.
  Ikumbukwe jana pia bao pekee la ushindi katika mchezo dhidi ya Mbao FC limefungwa na mchezaji wa kigeni pia, Mnamibia Sadney Urikhob.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KALENGO NJE MIEZI MITATU BAADA YA KUUMIA KWENYE MECHI YA KIRAFIKI DHIDI YA PAMBA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top