• HABARI MPYA

    Monday, October 21, 2019

    YANGA SC YAPUNGUZA VIINGILIO VYA MCHEZO WAKE NA PRYRAMIDS HADI SH 7,000 JUMAPILI KIRUMBA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KLABU ya Yanga imepunguza viingilio vya mchezo wake wa kwanza wa mchujo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pryramids FC ya Misri utakaofanyika Jumapili wiki hii kutoka Sh. 10,000 hadi Sh. 7,000 kwa eneo la mzunguko.
    Makamu Mwenyekiti wa Yanga SC, Frederick Mwakalebela amesema leo mjini Mwanza kwamba, hatua hiyo imefuatia maoni ya wanachama na mashabiki wa timu hiyo kutoka sehemu mbalimbali baada ya kutajwa viingilio hivyo awali. 
    Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela amesema kiingilio cha VVIP ambacho kilikuwa Sh. 70,000 nacho kimeshuka hadi 50,000 na kile cha VIP nacho kimeshuka kutoka 50,000 hadi Sh 20,000.
    Tulipofika hapa tulifanya vikao mbalimbali na wadau wa hapa Mwanza, pamoja na wawakilishi wa wanachama wetu kutoka mikoa ya jirani, tulipokea maoni yao kuhusu kiingilio na masuala mengine na kwakuwa Kamati ya Utendaji ya Yanga ni sikivu, kimsingi imeridhia mapendekezo ambayo yalitolewa na viongozi na wawakilishi wa Wanachama na mashakibi wetu,”amesema Mwakalebela.
    Amesema Uongozi wa Yanga umefurahishwa na ushiriki wa moja kwa moja wa wanachama na mashabiki kwenye shughuli za timu timu yao na amewapongeza sana kwa jinsi ambayo wametoa maoni yao kwa njia sahihi.
    “Kama Uongozi tumefarijika sana, na tunaamini kiingilio hiki sasa ni shirikishi kwa kuwa kimezingatia maoni ya moja moja kutoka kwa Wanachama na wapenzi wenyewe wa Yanga. Kilicho basi sisi kama Uongozi tunawaomba waje kwa wingi kuujaza Uwanja wa CCM Kirumba, washuhudie tunavyojenga historia kutokea katika jiji la Mwanza,” amesema.
    Mwakalebela amesema kwamba kambi ya timu imeendelea kuimarika mjini Mwanza huku kikosi kikiendelea vyema na mazoezi kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mbao FC kesho Uwanja wa CCM Kirumba.
    Wachezaji waliokuwa timu ya Taifa, Abdulaziz Makame na Metacha Mnata pamoja na Issa Bigirimana aliyekuwa mgonjwa  tayari wamejiunga na kikosi hapa Mwanza na baada ya mazoezi ya siku mbili Kocha Mkuu  wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema vijana wake wako tayari kwa mchezo huo.
    Kwa upande kocha Mkongo, Mwinyi Zahera amesema;“Kwa kawaida naiandaa timu kwa ajili ya mchezo uliokuwa mbele yangu, hadi sasa naona timu iko vizuri sana na iko tayari kwa mchezo dhidi ya Mbao FC. Tunawaheshimu Mbao ni timu nzuri, lakini na sisi ni wazuri pia na tumejiandaa kwa ushindi,”.
    Wachezaji walipo kambini jijini Mwanza ni pamoja na Papy Tshishimbi, David Molinga, Deus Kaseke, Ramadhan Kabwili, Faouk Shikalo, Sadney Urikhob, Juma Balinya, Mrisho Ngassa, Ally Mtoni Sonso, Muharami Issa ‘Marcelo’, Juma Abdul, Kelvin Yondani, Feisal Salum, Ally Ally, Jafari Mohammed, Gustafa Simon, Lamine Moro, Said Juma Makapu, Raphael Daudi, Maybin Kalengo, Mapinduzi Balama, Patrick Sibomana, Mustafa Seleman na Paul Godfrey.
    Naye Daktari Shecky Mgazija amesema wachezaji wote wa Yanga wako kwenye hali nzuri na utimamu wa mchezo hivyo ji jukumu la kocha tu kuwatumia katika mchezo dhidi ya Mbao FC Jumanne.
    Kuhusu hali ya beki wa kulioa wa timu hiyo Paul Godfrey ‘Boxer’ Dr. Mgazija amesema beki huyo anaendele vizuri na ataweza kuwa fiti kutumika katika mchezo dhidi ya Pyramids kama Mwalimu ataridhika na hali ya mazoezi yake. 
    “Kimsingi Boxer amepona, lakini hawezi kuingia moja kwa moja kikosini, hivyo anaendelea na mazoezi na ninamaamini baada ya kesho atajuika na wezake tayari kwa mchezo wa Pyramids kama atakuwa ameshaiva kwenye programu za kocha,”amesema Mgazija.
    Aidha amesema majeruhi mwengine Mohammed Issa ‘Banka’’ na Cleofas  Sospeter  bado hajajiunga na timu lakini matatibabu yake yanaendelea vizuri na huenda akajiunga na wenzake baada ya timu kurejea kutoka Misri.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC YAPUNGUZA VIINGILIO VYA MCHEZO WAKE NA PRYRAMIDS HADI SH 7,000 JUMAPILI KIRUMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top