• HABARI MPYA

  Jumatano, Oktoba 30, 2019

  SIMBA SC YAPUNGUZWA KAZI SHINYANGA, YACHAPWA 1-0 NA MWADUI FC KAMBARAGE

  Na Asha Said, SHINYANGA
  MABINGWA watetezi, Simba SC leo wamepunguzwa kasi baada ya kuchapwa 1-0 na wenyeji, Mwadui FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. 
  Kiboko ya Simba SC leo alikuwa ni mshambuliaji Gerald Mathias Mdamu aliyeifungia Mwadui FC bao hilo pekee la ushindi kwa kichwa dakika ya 32 akimalizia krosi ya Mussa Nampaka.
  Hicho kinakuwa kipigo cha kwanza msimu huu kwa mabingwa hao watetezi katika mchezo wa saba kikosi cha kocha Mbelgiji, Patrick Aussems kikitoka kushinda mechi zote sita za mwanzo.
  Pamoja na kuruhusu bao hilo moja, kipa Aishi Salum Manula akiidakia Simba SC mechi ya 100 tangu ajiunge nayo kutoka Azam FC Juni mwaka 2017 aliokoa michomo mingine mingi ya hatari. 
  Pamoja na kichapo hicho, Simba SC inayobaki na pointi zake 18, inaendelea kukaa kileleni mbele yanKagera Sugar ambayo baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Namungo FC leo Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba inafikisha pointi 16 baada ya kucheza mechi nane.
  Mabao ya Kagera Sugar unayofundishwa na Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Mecky Mexime yamefungwa na wachezaji wake wapya, Frank Ikobela aliyesajiliwa kutoka Mbeya City dakika ya 12 na Yusuphu Mhilu aliyesajiliwa kutoka Yanga dakika ya 69.
  Ndugu zao, Mtibwa Sugar nao wakaichapa Coastal Union 2-1 Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, mabao ya wenyeji yakifungwa na beki Dickson Daudi Mbekya dakika ya 20 ambaye pia alijifunga kuwapatia bao wageni na mshambuliaji Jaffar Salum Kibaya dakika ya 56.
  Nayo Lipuli FC ya Iringa ikawachapa Polisi Tanzania 2-1 Uwanja wa Samora mjini Iringa, mabao ya wenyeji yakifungwa na Kenneth Masumbuko dakika ya 34 na Paul Nonga dakika ya 74, huku bao pekee la wageni likifungwa na Mohamed Mkopi dakika ya 73.
  Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, bao pekee la Santos Mazengo dakika ya 17 likawapa ushindi wa 1-0 Ruvu Shooting dhidi ya KMC.
  Na mabao ya Danny Lyanga dakika ya 36 na Adam Adam dakika ya 41 yakawapa ushindi wa ugenini wa 2-1 JKT Tanzania dhidi ya wenyeji, Singida United ambao bao lao lilifungwa na Ramadhan Hashim dakika ya 55. 
  Kikosi cha Mwadui FC kilikuwa; Mahamoud Amiri, Rogers Gabriel, Augustino Samson, Joram Mgeveke, Emmanuel Membe, Hassan Kapalata, Mussa Kampaka, Omar Daga, Gerald Mathias na Ludovck Evance. 
  Simba SC; Aishi Manula, Haruna Shamte, Erasto Nyoni, Tiarone Santos, Gerson Fraga ‘Viera’, Clatous Chama/Miraji Athuman ‘Madenge’ dk46, Muzamil Yassin, Meddie Kagere, Sharaf Eldin Shiboub na Francis Kahata/Ibrahim Ajibu dk60.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAPUNGUZWA KAZI SHINYANGA, YACHAPWA 1-0 NA MWADUI FC KAMBARAGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top