• HABARI MPYA

    Tuesday, October 09, 2018

    TAIFA STARS YAWAFUATA CAPE VERDE BILA MKUDE, DANTE NA DOMAYO…AMUNIKE ABEBA MAKIPA WANNE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mnigeria, Emmanuel Amunike ameongeza makipa wawili, Aaron Kalambo wa Tanzania Prisons na Benedicto Tinocco wa Mtibwa Sugar katika kikosi cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kinachoondoka usiku huu kwenda Praia nchini Cape Verde.
    Na hao wanaungana na makipa wengine wawili, Aishi Manula wa Simba SC na Beno Kakolanya wa Yanga kwa safari leo, baada ya kuachwa kwa Mohammed Abdulrahman wa JKT Tanzania ambaye ameumia.
    Pamoja na Abdulrahman, Amunike pia amewatema beki Andrew Vincent ‘Dante na viungo Jonas Mkude na Frank Domayo kwa sababu wote ni majeruhi, wakati kiungo Salum Kihimbwa na mshambuliaji Kelvin Sabato wameachwa kwa sababu za kiufundi.
    Beki Andrew Vincent 'Dante' hatasafiri na Taifa Stars usiku huu kwenda Praia kwa sababu ni majeruhi 

    Viungo wengine, Simon Msuva wa Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco, Farid Mussa na washambuliaji Shaaban Iddi Chilunda wote wa CD Tenerife ya Hispania na Nahodha Mbwana Ally Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji wap watajiunga na timu moja kwa moja mjini Praia kesho Alfajiri.
    Wachezaji wengine wote wanaocheza nje, mabeki; Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia, Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini, kiungo Himid Mao wa Petrojet ya Misri na washambuliaji Thomas Ulimwengu wa Al Hilal ya Sudan na Rashid Mandawa wa BDF XI ya Botswana wataondoka pamoja na wengine wanaocheza nchini usiku wa leo.
    Taifa Stars watakuwa wageni wa Cape Verde katika mchezo wa Kundi L kufuzu AFCON Oktoba 12 mjini Praia kabla ya kurejea Dar es Salaa kwa mchezo wa marudiano na wapinzani wao hao Oktoba 16.
    Taifa Stars iliyokuwa imeweka kambi katika hoteli ya Sea Scape iliyopo Kunduchi mjini Dar es Salaam ilikuwa ikifanya mazoezi Uwanja wa JMK Centre, eneo la Gerezani katikati ya Jiji chini ya Kocha Mkuu, Amunike, anayesaidiwa na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi, na wazalendo Hemed Suleiman ‘Morocco’, Meneja Danny Msangi, Mtunza Vifaa ni Ally Ruvu na Madaktari Richard Yomba na Gilbert Kigadya.
    Tanzania inashika nafasi ya tatu katika Kundi L ikiwa na pointi mbili tu baada ya sare zote katika mechi zake mbili za mwanzo, 1-1 na Lesotho nyumbani mwaka jana na 0-0 na Uganda ugenini mapema mwezi huu.
    Uganda wanaendelea kuongoza Kundi hilo kwa pointi zao nne, wakifuatiwa na Lesotho mbili sawa na Tanzania na mabao mawili ya kufunga, wakati Cape Verde wanashika mkia kwa pointi yao moja. 
    Kihistoria Tanzania imecheza fainali moja tu za AFCON, mwaka 1980 nchini Nigeria, tena enzi hizo bado zinajulikana kama Fainali za kombe la Mataifa Huru ya Afrika.
    Kikosi kizima cha Stars kinachotarajiwa kuwasili Praia kesho kinaundwa na makipa; Aishi Manula (Simba SC), Beno Kakolanya (Yanga SC), Aaron Kalambo (Tanzania Prisons) na Benedicto Tinocco (Mtibwa Sugar Tanzania).
    Mabeki; Hassan Kessy (Nkana FC/Zambia), Shomari Kapombe (Simba SC), Salum Kimenya (Tanzania Prisons), Gardiel Michael (Yanga SC), Paulo Ngalema (Lipuli FC), Ally Sonso (Lipuli FC), Aggrey Morris (Azam FC), David Mwantika (Azam FC), Abdallah Kheri (Azam FC), Kelvin Yondani (Yanga SC) na Abdi Banda (Baroka FC).
    Viungo ni Himid Mao (Petrojet/Misri), Simon Msuva (Difaa Hassan El –Jadida/Morocco), Mudathir Yahya (Azam FC), Feisal Salum (Yanga SC) na Farid Mussa (CD Tenerife/Hispania).
    Washambuliaji; Mbwana Samatta (Nahodha, KRC Genk/Ubelgiji), Thomas Ulimwemgu (Al Hilal/Sudan), John Bocco (Simba SC), Yahya Zayed (Azam), Kelvin Sabato (Mtibwa Sugar), Rashid Mandawa (BDF XI/Botswana) na Shaaban Iddi Chilunda (CD Tenerife/Hispania).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAIFA STARS YAWAFUATA CAPE VERDE BILA MKUDE, DANTE NA DOMAYO…AMUNIKE ABEBA MAKIPA WANNE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top