• HABARI MPYA

    Friday, October 19, 2018

    DAKTARI AFRIKA KUSINI AAMUA FRANK DOMAYO APUMZIKE SOKA KWA MIEZI MINNE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    NAHODHA Msaidizi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Frank Domayo ‘Chumvi’, anatarajia kukaa nje ya dimba kwa muda wa miezi minne sawa na wiki 16.
    Domayo aliyekuwa kwenye uchunguzi jijini Cape Town, Afrika Kusini wiki iliyopita, atakuwa nje ya dimba kwa kipindi hicho chote baada ya kugundulika ana majeraha kwenye goti lake baada ya kuchana mtulinga wa nyuma wa goti lake la mguu wa kulia (posterior cruciate ligament).
    Kiungo huyo alipata majeraha hayo akiwa na timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, iliyokuwa ikijiandaa na mechi mbili za kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika nchini Cameroon mwakani dhidi ya Cape Verde.
    Daktari Mkuu wa Azam FC, Dr. Mwanandi Mwankemwa, amesema kwamba tayari amepokea ripoti kutoka Afrika Kusini, ambayo inaeleza kuwa kiungo huyo atakuwa nje ya dimba kwa muda wa miezi minne kabla ya kurejea kwenye ushindani.

    Frank Domayo ‘Chumvi’ anatakiwa kuwa nje ya Uwanja kwa muda wa miezi minne 

    “Frank Domayo alipatwa na maumivu ya goti akiwa mazoezini katika timu yetu ya Taifa wiki moja na nusu iliyopita na kwa ushirikiano uliopo kwa klabu na timu yetu ya Taifa alifanyiwa vipimo vya M.R.I katika Kliniki ya Besta na vilevile High Tech na baadaye baada ya kugundulika amepata tatizo kidogo la ligament (mtulinga) uongozi wa timu ya Azam uliamua kumpeleka Afrika Kusini, Cape Town katika Hospitali ya Vincent Pallotti kwa matibabu zaidi.
    “Baada ya kwenda ilibainika kweli amepata majeraha ya Posterior Cruciate Ligament yaani mtulinga uliopo nyuma ya goti lake la kulia na Domayo hajakatika ligament yote bali ni sehemu ya ligament na hiyo Posterior Cruciate Ligament taratibu za matibabu yake inaweza kupona bila kufanyiwa upasuaji,” alisema.
    Mwankemwa alisema kuwa kutokana na majeraha hayo, Domayo kwa kipindi cha miezi mitatu atatakiwa kufanya mazoezi ya ‘physiotherapy’.
    “Kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa Domayo atatakiwa kufanya mazoezi ya Physiotherapy, hasa msisitizo wa kuimarisha misuli yake ya paja ambayo na katika miezi mitatu anakatazwa kukimbia na kufanya mazoezi ya kichura ‘squat’ lakini baada ya miezi mitatu kupita kuanzia sasa ataanza tena kukimbia na baada ya miezi minne ndio Frank Domayo atarudi tena uwanjani,” alisema.
    Aliongeza kuwa: “Hiki kipindi ambacho anaimarisha misuli ya paja anaruhusiwa kufanya mazoezi ya baiskeli lakini sio mazoezi ya kukimbia.”
    Katika hatua nyingine, Mwankemwa alimzungumzia mshambuliaji Paul Peter, aliyeongozana na Domayo kwa ajili ya uchunguzi na kusema kuwa muda wowote kuanzia sasa wanatarajia kutuma ripoti yake kamili muda wowote kuanzia sasa baada ya kufanyiwa upasuaji mdogo wa goti jana Alhamisi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: DAKTARI AFRIKA KUSINI AAMUA FRANK DOMAYO APUMZIKE SOKA KWA MIEZI MINNE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top