• HABARI MPYA

    Sunday, October 21, 2018

    TUNAONA KAMA TAIFA STARS IMEKWISHAFUZU FAINALI ZA KOMBE LA MATAIFA YA AFRIKA MWAKANI NCHINI CAMEROON, WAKATI...

    TANZANIA imefufua matumaini ya kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon kufuata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde kwenye mchezo wa Kundi L Jumanne Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Ushindi huo ulikuja siku tatu baada ya Taifa Stars kufungwa mabao 3-0 na Papa wa Bluu katika mchezo wa kwanza mjini Praia Oktoba 12 na kuwatia simanzi kubwa Watanzania.
    Ushindi huo wa kwanza kwenye mashindano haya, unaifanya Taifa Stars ijisogeze hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi hilo, ikifikisha pointi tano baada ya kucheza mechi nne, ikifungwa moja na sare mbili. 
    Uganda ambayo siku hiyo iliifunga tena Lesotho 2-0 mjini Maseru, ndiyo inaongoza kundi hilo kwa pointi zake 10 za mechi nne, wakati Cape Verde inabaki na pointi zake nne katika nafasi ya tatu. Lesotho ndiyo inashika mkia kwa pointi zake mbili. 


    Shujaa wa Tanzania Jumanne alikuwa Nahodha Mbwana Ally Samatta anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji aliyefunga bao moja na kuseti moja katika ushindi huo, ingawa pia alikosa penalti. 
    Samatta alianza kumsetia kiungo mshambuliaji wa Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco, Simon Msuva dakika ya 29 kabla ya yeye mwenyewe kufunga bao la pili dakika ya 58 kwa shuti la mbali baada ya pasi ya kiungo wa Azam FC, Mudathir Yahya Abbas.
    Awali, dakika ya 22 Samatta aligongesha mwamba wa juu mkwaju wa penalti uliotolewa na refa Michael Gasingwa wa Rwanda baada ya beki wa MOL Vidi FC ya Hungary Ianique dos Santos Tavares ‘Stopira’ kumuangusha Msuva kwenye boksi.
    Taifa Stars itasafiri kuifuata Lesotho mwezi ujao kabla ya kukamilisha mechi za Kundi L kwa kumenyana na Uganda Machi mwakani, miezi miwili tu kabla ya kuanza kwa AFCON ya mwakani.  
    Uganda wanahitaji pointi moja kutoka kwenye mechi zao mbili zilizobaki, dhidi ya Cape Verde nyumbani na Tanzania ugenini ili kujihakikishia tiketi ya AFCON za pili mfululizo.
    Kwa sasa Cape Verde wanaweza kufikisha pointi 10 iwapo watashinda mechi zao mbili zilizosalia dhidi ya Uganda ugenini na Losotho nyumbani.
    Lesotho wanaweza kufikisha pointi nane iwapo watashinda mechi zao mbili zilizobaki dhidi ya Tanzania nyumbani kwao na dhidi ya Cape Verde ugenini. 
    Nasi, Tanzania tunaweza kufikisha pointi 11 iwapo tutashinda mechi zote zilizosalia, dhidi ya Lesotho ugenini na Uganda hapa nyumbani.
    Utaona kila timu ina nafasi ya kufuzu AFCON katika kundi L kama itafanya vizuri katika mechi zake zijazo na hata Uganda mwenyewe bado hajajihakikishia tiketi.
    Uganda haitafuzu iwapo itafungwa mechi zote zilizobaki na Tanzania na Cape Verde zikashinda mechi zao zote zilizobaki.
    Hii maana yake, bado shughuli pevu katika Kundi L na huu si wakati wa kuanza shangwe, sherehe, maandalizi ya kushiriki AFCON ambayo hatujafuzu.
    Bali huu ni wakati wa kuweka mipango ya kukusanya pointi katika mechi mbili zijazo, tukifikiria ugumu uliopo mbele yetu.
    Leo hii Watanzania, hususan viongozi wetu wanaona na wanaamini wana kazi nyepesi sana kuelelea AFCON baada ya kushinda mechi moja tu, wakati hao Uganda walioshinda mechi tatu wanaihisi shughuli pevu iliyopo mbele yao na wajapinga sawasawa.
    Tunaona ni kazi nyepesi kuifunga Lesotho kule Maseru, tu kwa sababu imefungwa na Uganda pale pale – lakini hatujiulizi hiyo ndiyo timu ambayo tulishindwa kuifunga hapa nyumbani kwetu.
    Mawazo kama haya yalitufanya tukafungwa 3-0 na Cape Verde katika mechi ambayo tungeweza japo kupata sare kama tungecheza kwa nidhamu iliyostahili.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TUNAONA KAMA TAIFA STARS IMEKWISHAFUZU FAINALI ZA KOMBE LA MATAIFA YA AFRIKA MWAKANI NCHINI CAMEROON, WAKATI... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top