• HABARI MPYA

  Sunday, October 28, 2018

  TUMPOKEE NINJE NA KUMPA USHIRIKIANO KWA MANUFAA YA TAIFA LETU

  UTEUZI wa Ammy Conrad Ninje kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) umeibua maswali miongoni mwa wadau wa michezo nchini, juu ya sifa za mwalimu huyo wa muda mfupi wa timu mbalimbali za taifa nchini.
  Maswali yanafanana juu ya shaka ya Ninje kupewa nafasi hiyo na kubwa ni kuhusu uwezo na tabia zake baada ya muda mfupi wa kupewa nafasi katika timu za taifa.
  Ninje amechukua nafasi ya Oscar Milambo aliyekuwa anakaimu nafasi hiyo kwa muda tangu katikati ya mwaka kufuatia Salum Madadi kubadilishiwa majukumu.
  Mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars anapewa Ukurugenzi wa Ufundi baada ya kuwa Kocha wa timu mbalimbali za taifa za vijana na wakubwa.
    
  Alianza kama Kocha Msaidizi wa Taifa Stars chini ya mzalendo mwenzake, Salum Mayanga mwaka jana kabla ya kupandishwa na kuwa kocha wa kikosi cha Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ kilichoshiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Challenge nchini Kenya mwaka jana.
  Pamoja na Kilimanjaro Stars kufanya vibaya kwenye michuano hiyo, Ninje akapandishwa kuwa kocha wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes ambayo nayo haikuwa na matokeo mazuri baada ya kutolewa mapema kwenye mechi za kufuzu AFCON U20 mwakani Niger.
  Kihistoria Ammy Ninje alizaliwa mwaka 1978, Dar es Salaam, Tanzania na alianza shule msingi Bunge iliyopo Jiji Kuu la Tanzania,  kuanzia mwaka 1985 – 1991.
  Alisoma shule ya Sekondari ya Kilimanjaro 1992 na baadaye alijiunga kidato cha tano na sita Shule ya Sekondari ya Al-Haramain, Kariakoo jijini.
  Alianza kucheza soka katika timu ya Boom FC ya Ilala na baadaye Manyema FC zote za Dar es Salaam kabla ya kujiunga JKT Ruvu wakati huo inaitwa 832 KJ Ruvu.
  Baadaye alikwenda kucheza soka Afrika Kusini kwenye timu za Hellenic FC na kisha Wynberg St Jones kabla  ya kujiunga na Sparta Rotterdam (Mutual) FC ya China pia alicheza katika nchi za Denmark, USA, Scotland na England.
  Ninje, ambaye kitaalum ni Mhasibu, amewahi kucheza timu ya Taifa ya Tanzania katika vipindi tofauti wakati inafundishwa na Kocha mzawa Dk. Mshindo Msolla kabla ya kuanza kufundisha soka katika chuo cha Hull mwaka 2007 hadi 2010.
  Amefundishwa pia timu ya watoto ya shule ya Msingi ya Collingwood kati ya 2009 na 2013, Soccer kati ya 2012 na 2014, Notts County FC kati ya 2013 hadi mwaka jana aliporejea nyumbani Tanzania na kuanza kufundisha timu za taifa.
  Milambo alikaimu nafasi hiyo kwa muda mfupi, lakini hakukuwa na shaka juu ya uwezo wa watangulizi wao, Sunday Burton Kayuni na Madadi. 
  Jirani zetu, Kenya wamemuajiri Mromania mzaliwa wa Ujerumani, Andreas Spier kuwa Mkurugenzi wao wa Ufundi.
  Hakuna kingine Shirikisho la Soka Kenya (FKF) kilitazama kwa mtaalamu huyo zaidi ya sifa zake na uzoefu wa kufanya kazi katika nchi kadhaa za Afrika.
  Spier mwenye umri wa miaka 54 alikuwa kocha wa timu ya taifa ya vijana ya Romania chini ya umri wa miaka 19 kuanzia mwaka 2014 hadi Aprili 2016.
  Baadaye akaja Afrika kufundisha timu ya taifa ya wanawake ya Rwanda mwaka 2008 kabla ya kuhamia APR FC ambako alipewa timu ya vijana, ambayo mwaka mmoja baadaye ilipewa jina Intare FC.
  Mwaka 2013 akapewa timu ya wakubwa ya APR ambayo aliifundisha hadi Aprili 2014 kabla ya kuondoka kufuatia kukasirika kwa kufungiwa mechi tano baada ya kukosoa uamuzi wa refa katika mechi ya Ligi Kuu Rwanda.
  Wakurugenzi wa awali wa Ufundi wa FKF kabla ya Spier walikuwa Jacob ‘Ghost’ Mulee na Patrick Naggi, wote wachezaji na makocha wa zamani w Harambee Stars, tena wa kiwango cha juu kama Kayuni na Madadi kwa Tanzania.
  Ni kwa mifano hii ndiyo maana watu wanahoji Ninje kupewa nafasi hiyo, wakikumbuka migogoro yake na wachezaji wakati wa michuano ya CECAFA Challenge nchini Kenya hadi timu ikapata matokeo mabaya ya kihistoria – yaani haijawahi kutokea ilitolewa bila kushinda hata mechi moja.
  Na hata Ngorongoro Heroes alitofautiana na kipa Ramadhani Kabwili bila sababu za msingi, kijana aliitwa na klabu yake akahesabiwa ametoroka kambini na kufukuzwa kwenye timu yake matokeo yake akadaka kipa asiye na uzoefu dhidi ya Mali timu ikafungwa kirahisi na kutolewa.   
  TFF, chini ya Rais wake, Wallace Karia  ndiyo yenye mamlaka ya kuamua nani apewe nafasi gani kwa sababu wao ndiyo waliopewa dhamana na Wajumbe wa Mkutano Mkuu kuongoza soka ya Tanzania – hivyo kelele za kupinga uteuzi wa Ninje ni kazi bure.
  Tumpokee Ninje kama mtu muhimu aliyepewa majukumu mazito kwa mustakabali wa soka ya Tanzania na kumpa ushirikiano kwa manufaa ya taifa letu – kwa sababu hakuna namna nyingine.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TUMPOKEE NINJE NA KUMPA USHIRIKIANO KWA MANUFAA YA TAIFA LETU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top