• HABARI MPYA

  Ijumaa, Oktoba 26, 2018

  ‘PANGA PANGUA’ RATIBA LIGI KUU YAENDELEA, SAFARI HII MECHI ZA VIGOGO ZAAHIRISHWA SABABU YA TAIFA STARS

  Na Nasra Shomari, DAR RS SALAAM
  MECHI za Ligi Kuu ya Tanzania Bara zinazozihusu Azam, Simba na Yanga zilizopangwa kufanyika wiki ya kwanza ya Novemba zimeahirishwa kupisha maandalizi ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kuelekea mechi dhidi ya Lesotho Novemba 18, mwaka huu kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
  Mechi hizo ni kati ya African Lyon na Yanga iliyopangwa kufanyika Novemba 7, Simba SC na KMC FC na Azam FC na Mbao FC zote Novemba 8, mwaka huu mjini Dar es Salaam.
  Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB), Boniphace Wambura Mgoyo amesema kwamba kutokana na umuhimu wa timu ya taifa, ndio maana wameamua kusogeza mbele michezo hizo ili kupisha maandalizi hayo.

  Emmanuel Okwi wa Simba SC akimpita mchezaji wa Alliance FC katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu

  Amesema kwamba kwa sababu kiu ya kila Mtanzania kwa sasa ni kuona Taifa Stars inakata tiketi ya kucheza AFCON, ndiyo maana Bodi ya Ligi imeamamua kuondoa mechi hizo ili wachezaji waweze kupata muda wa kutosha wa maandalizi katika kambi ya Afrika Kusini.
  Lakini pia Wambura amesema kwamba mechi tatu za viporo nazo zimepangiwa tarehe, ambazo ni Novemba 21 Yanga SC na Mwadui FC Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Simba SC na Lipuli FC Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam Novemba 22, Azam na Ruvu Shootin Uwanja wa Azam Complex Chamazi.
  Baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Cape Verde Oktoba 16 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Taifa Stars sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi L kuwania tiketi ya Cameroon mwakani, ikifikisha pointi tano baada ya kucheza mechi nne, ikifungwa moja na sare mbili. 
  Uganda ambayo siku hiyo iliifunga tena Lesotho 2-0 mjini Maseru, ndiyo inaongoza kundi hilo kwa pointi zake 10 za mechi nne, wakati Cape Verde inabaki na pointi zake nne katika nafasi ya tatu. Lesotho ndiyo inashika mkia kwa pointi zake mbili.   
  Taifa Stars itasafiri kuifuata Lesotho Novemba 18 mjini Maseru kabla ya kukamilisha mechi za Kundi L kwa kumenyana na Uganda Machi 22 mwakani, miezi miwili tu kabla ya kuanza kwa AFCON ya mwakani.   
  Na jana Serikali kupitia kwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe imetangaza harambee ya kuichangia Taifa Stars ikaweke kambi Afrika Kusini kujiandaa na mchezo dhidi ya Lesotho mjini Maseru katikati ya mwezi ujao.
  Aidha, Waziri Mwakyembe amesema Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na TFF watahakikisha Taifa Stars inapata kambi nzuri nchini Afrika Kusini na salama kuelekea mchezo dhidi ya Lesotho.
  Mwakyembe alisema bajeti ya maandalizi ya Taifa Stars imeongezeka kwa zaidi ya nusu hadi Sh. Milioni 350 baada ya uamuzi wa kambi ya Afrika Kusini.
  Wakati huo huo: Wambura amesema kwamba mkutano wa tano wa Baraza Kuu la TPLB utafanyika Desemba 1, mwaka huu mjini Tanga, ajenda zikiwa ni pamoja na kujaza nafasi zilizoachwa na wazi viongozi waliojiuzulu akiwemo Mwenyekiti na Wajumbe wawakilishi wa klabu za Ligi Daraja la kwanza na Ligi Daraja la Pili.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ‘PANGA PANGUA’ RATIBA LIGI KUU YAENDELEA, SAFARI HII MECHI ZA VIGOGO ZAAHIRISHWA SABABU YA TAIFA STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top