• HABARI MPYA

  Wednesday, October 24, 2018

  SIMBA SC WANAMENYANA NA ALLIANCE FC LEO WAKISHINDA WATAIPITA YANGA KWENYE MSIMAMO WA LIGI KUU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MABINGWA watetezi, Simba SC leo wanateremka Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kumenyana na Alliance FC ya Mwanza katika mfululizo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakitafuta ushindi ili wapande juu ya mahasimu wao, Yanga.
  Hiyo itakuwa mechi moja tu kati ya tano za leo, nyingine zikiwa ni kati ya Coastal Union na Kagera Sugar Uwanja wa Mwakwani mjini Tanga Saa 8:00 mchana, JKT Tanzania na Azam FC Uwanja wa Meja Isamuhyo, Mbweni mjini Dar es Salaam, Tanzania Prisons na African Lyon Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na Ruvu Shooting na Singida United Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, zote Saa 10:00 jioni.
  Lakini macho na masikio ya wengi yataelekezwa Uwanja wa Taifa Saa 1:00 usiku ambako mabingwa watetezi watakuwa wanafanya mambo yao.
  Simba SC ikishinda leo itafikisha pointi 20 na kuivuka Yanga kwenye msimamo wa Ligi Kuu

  Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Patrick Aussems itaingia kwenye mchezo huo, wakitoka kuipa kichapo cha 3-0, timu nyingine ya Kanda ya Ziwa, Stand United ya Shinyanga.
  Na Alliance FC ya kocha Mbwana Makatta baada ya kukaribishwa mjini kwa kipigo cha 3-0 Jumamosi na Yanga, leo watakuwa wanacheza Uwanja wa Taifa kwa mara ya pili tu. 
  Mechi nyingine za Ligi Kuu zitafuatia kesho, Mbeya City wakiwa wenyeji wa Mwadui FC ya Shinyanga Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya Saa 8:00 mchana, Stand United wakiwakaribisha Mtibwa Sugar ya Morogoro Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Ndanda FC wakiwakaribisha Biashara United ya Mara Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, Mbao FC wakiwa wenyeji wa  Lipuli FC ya Iringa zote Saa 10:00 jioni.
  Mechi za katikati ya wiki zitakamilishwa kwa mchezo baina ya wana Dar es Salaam watupu, KMC FC ya Kinondoni dhidi ya Yanga SC ya Kariakoo, Manispaa ya Ilala iliyotapakaa nchi nzima ambao utaanza Saa 1:00 usiku Uwanja wa Taifa.
  Hadi sasa Azam FC ndiyo wanaongoza Ligi Kuu kwa pointi zao 21 za mechi tisa, wakifuatiwa na Yanga SC yenye pointi 19 za mechi saba, wakati Simba SC ina pointi 17 za mechi nane.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC WANAMENYANA NA ALLIANCE FC LEO WAKISHINDA WATAIPITA YANGA KWENYE MSIMAMO WA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top