• HABARI MPYA

  Jumanne, Oktoba 30, 2018

  YANGA SC YAREJEA NAFASI YA PILI LIGI KUU BAADA YA KUIPIGA LIPULI FC 1-0 BAO PEKEE LA MAKAMBO TAIFA

  Na Nasra Omar, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Yanga SC imerudi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Lipuli FC ya Iringa usiku huu Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Shukrani kwa mfungaji wa bao hilo pekee, mshambuliaji Heritier Makambo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) dakika ya tisa tu akimalizia pasi ya kiungo mzawa, Mrisho Ngassa.
  Ngassa alipokea pasi ndefu ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ na akamtoka vizuri beki Paul Ngalema kabla ya kuingia ndani kidogo na kumpasia Makambo aliyekuwa anatazamana na nyavu akafunga kiulaini.

  Kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 25 baada ya kucheza mechi tisa na kurudi nafasi ya pili, ikiwaangushia nafasi ya tatu mabingwa watetezi, Simba SC wenye pointi 23 za mechi 10 – na Azam FC inaendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 27 ikiwa imecheza mechi 11. 
  Yanga SC ingeweza kuibuka na ushindi mtamu zaidi kama ingetumia nafasi zake nyingine ilizotengeneza na kilichowakwamisha leo ni uimara wa safu ya ulinzi ya Lipuli iliyoongozwa na beki Mganda, Joseph Owino.
  Beki mkongwe, Kelvin Yondan aliiongoza vyema safu ya ulinzi ya Yanga kuwazuia kabisa Lipuli, ambao safu yao ya ushambuliaji iliongozwa na Paul Nonga, ambaye dakika 49 alipiga shuti kali baada ya pasi ya Seif Abdallah Karihe lililookolewa na kipa, Beno Kakolanya.
  Yanga SC ilipata pigo dakika ya 82 baada ya beki wake wa kulia, Paul Geoffrey kutolewa kwa kadi nyekundu, kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njana, baada ya kumchezea rafu Miraj Athumani ‘Madenge’.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Beno Kakolanya, Paul Geoffrey, Gardiel Michael,  Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Mrisho Ngassa/Juma Abdul dk87, Maka Edward, Herithier Makambo, Thabani Kamusoko/Said Juma ‘Makapu’ dk71 na Matheo Antony/Deus Kaseke dk66.
  Lipuli FC: Mohamed Yusuph, Wiliam ‘Gallas’ Lucian/Daruwesh Saliboko dk86, Paul Ngelema, Ibrahim Job/Yussuf Waheed dk71, Joseph Owino, Novarty Lufunga, Miraji Athumani, Jimmy Shoji Mwasondola/Seif Abdallah Karihe dk33, Paul Nonga, Issa Rashid na Zawadi Mauya.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC YAREJEA NAFASI YA PILI LIGI KUU BAADA YA KUIPIGA LIPULI FC 1-0 BAO PEKEE LA MAKAMBO TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top