• HABARI MPYA

  Saturday, October 20, 2018

  AJIB ASETI MABAO MAWILI NA KUFUNGA MOJA ZURI YANGA IKIISHINDILIA 3-0 ALLIANCE FC TAIFA

  Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
  KIKOSI cha Yanga SC kimeendelea kuwapa faraja mashabiki wake baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Alliance FC jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Kwa ushindi huo uliotokana na mabao ya mshambuliaji Mkongo, Heritier Makambo na wazalendo Mrisho Ngassa na Ibrahim Ajib, Yanga SC inafikisha pointi 19 baada ya kucheza mechi saba, sasa wakipanda nafasi ya pili nyuma ya Azam FC yenye pointi 21 za mechi tisa.
  Yanga SC wanawazidi kwa pointi tano mabingwa watetezi, SImba SC wenye pointi 14 za mechi saba, nyuma ya Singida United yenye pointi 17 za mechi 10.
  Mkongo, Makambo aliye katika msimu wake wa kwanza tu Yanga SC alianza kufunga bao la kwanza dakika ya 18 akimalizia kwa kichwa krosi ya Ibrahim Ajib aliyepasiwa na mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe.

  Kiungo mshambuliaji, Ibrahim Ajib (kushoto) akishangilia na Mkongo Heritier Makambo baada ya kazi nzuri leo

  Ajib tena akampa pasi ndefu mkongwe, Mrisho Khalfan Ngasa kuifungia Yanga SC bao la pili dakika ya 25 akimtungua kiufundi kocha wa Alliance FC.
  Ajib mwenyewe akajihakikishia uchezaji Bora wa Mechi kwa kufunga bao zuri la tatu dakika ya 86 kwa shuti la mbali kudogo baada ya kupokea pasi ya mbali ya kiungo Deus Kaseke aliyetokea benchi kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Ngassa.  
  Yanga SC wakaonekana kutosheka na mabao hayo na kuanza kucheza kwa madoido, pasi nyingi na wachezaji kuonyesha uwezo wao wa kumiliki mpira kwa madaha. 
  Mechi nyingine za leo, Tanzania Prisons imelazimishwa sare ya bila kufungana na Singida United ya Singida Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya sawa na Coastal Union iliyotoka 0-0 pia na JKT Tanzania ya Dar es Salaam Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga. 
  Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi nyingine tatu, mabingwa watetezi, Simba SC wakiwakaribisha Stand United Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Lipuli FC wakiwakaribisha Kagera Sugar ya Bukoba Saa 8:00 mchana Uwanja wa Samora mjini Iringa na Mbao FC wakiwa wenyeji wa Mtibwa Sugar ya Morogoro Saa 10: 00 jioni Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa: Beno Kakolanya, Paul Godfrey, Gardiel Michael, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Kelvin Yondan/Thabani Kamusoko dk77, Papy Kabamba Tshishimbi, Mrisho Ngassa/Deus Kaseke dk61, Raphael Daudi/Said juma ‘Makapu’ dk55, Heritier Makambo, Amissi Tambwe na Ibrahim Ajib.
  Alliance: Ibrahim Isihaka, Israel Patrick, Hance Masoud, Wema Sadoki, Geofrey Lusekeki, Joseph James, Juhudi Philemon/Jamal Mtengeta dk52, Balama Mapinduzi/Zabron Khamis dk77, Michael Chinedu, Siraji Juma/Dickson Ambundo dk49 na Juma Nyangi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AJIB ASETI MABAO MAWILI NA KUFUNGA MOJA ZURI YANGA IKIISHINDILIA 3-0 ALLIANCE FC TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top