MABINGWA watetezi, Yanga SC wameibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji, Mashujaa FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Lake Tangnyika mjini Kigoma.
Mabao ya Yanga SC leo yote yamefungwa na wachezaji wazawa, kiungo Mudathir Yahya Abbas dakika ya 28 na beki bakari Nondo Mwamnyeto ambaye pia ni nahodha wa timu hiyo, dakika 90’+2.
Kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 63 katika mchezo wa 26 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi tano Zaidi ya watani wao, Simba SC ambao hata hivyo wana mechi moja mkononi na kesho wanacheza na Pamba Jiji FC nyumbani, Dar es Salaam.
Kwa upande wao Mashujaa baada ya kupoteza mchezo huo wanabaki na pointi zao 27 za mechi 26 pia nafasi ya 11 katika Ligi Kuu inayoshirikisha timu 16.
Ikumbukwe mwisho wa msimu timu mbili zitashuka Daraja moja kwa moja, wakati nyingine mbili zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.
Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu kutoka Ligi ya Championship katika mechi nyingine mbili za mchujo nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ndiye atacheza Ligi Kuu msimu ujao.



.png)
0 comments:
Post a Comment