• HABARI MPYA

    Tuesday, October 09, 2018

    YALIKUWA MAKOSA MAKUBWA KUWATOA WACHEZAJI KAMBINI TAIFA STARS KWENDA KUZICHEZEA KLABU

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    NGUVU za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa sasa zimeelekezwa kwenye kuhakikisha timu ya taifa, Taifa Stars inafuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon.
    Taifa Stars watakuwa wageni wa Cape Verde katika mchezo wa Kundi L kufuzu AFCON Oktoba 12 mjini Praia kabla ya kurejea Dar es Salaam kwa mchezo wa marudiano na wapinzani wao hao Oktoba 16.
    Wachezaji wote wanaocheza nyumbani wapo kambini katika hoteli ya Sea Scape iliyopo Kunduchi mjini Dar es Salaam pamoja na mmoja anayecheza nje, Thomas Ulimwengu wa El Hilal ya Sudan wakiwa wanaendelea na mazoezi chini ya Kocha Mkuu Emmanuel Amunike, anayesaidiwa na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi, na wazalendo Hemed Suleiman ‘Morocco’, Meneja Danny Msangi, Mtunza Vifaa ni Ally Ruvu na Madaktari Richard Yomba na Gilbert Kigadya.
    Ambao hawajaripoti ni mabeki Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia na Abdi Banda Baroka FC ya Afrika Kusini, viungo Himid Mao wa Petrojet ya Misri, Simon Msuva wa Difaa Hassan El –Jadida ya Morocco na Farid Mussa wa CD Tenerife ya Hispania na washambuliaji Nahodha Mbwana Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji, Rashid Mandawa wa BDF XI ya Botswana na Shaaban Iddi Chilunda wa CD Tenerife ya Hispania.
    Wachezaji wa Yanga walioondolewa kambini Taifa Stars kwenda kuichezea klabu yao Jumapili kutoka kulia, Andrew Vincent 'Dante', Benno Kakolanya na Kelvin Yondan

    Tanzania inashika nafasi ya tatu katika Kundi L ikiwa na pointi mbili tu baada ya sare zote katika mechi zake mbili za mwanzo, 1-1 na Lesotho nyumbani mwaka jana na 0-0 na Uganda ugenini mapema mwezi huu.
    Uganda wanaendelea kuongoza Kundi hilo kwa pointi zao nne, wakifuatiwa na Lesotho mbili sawa na Tanzania na mabao mawili ya kufunga, wakati Cape Verde wanashika mkia kwa pointi yao moja. 
    Kihistoria Tanzania imecheza fainali moja tu za AFCON, mwaka 1980 nchini Nigeria, tena enzi hizo bado zinajulikana kama Fainali za kombe la Mataifa Huru ya Afrika.
    Lakini Taifa Stars ikiwa kambini, baadhi ya wachezaji waliruhusiwa kwenda kuzitumikia klabu zao kwenye mechi za Ligi Kuu na kurejea baada ya michezo husika.
    Jumapili wachezaji wawili Yanga SC, kipa Benno Kakolanya na Andrew Vincent ‘Dante’ waliumia katika mchezo dhidi ya Mbao FC Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam na kutolewa kwa machela kipindi cha pili nafasi zao zikichukuliwa na kipa Mkongo, Klaus Kindoki na beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’.
    Lakini mabeki wengine, Gardiel Michael na Kelvin Yondan ambao kama Kakolanya na Dante wapo Taifa Stars nao walimaliza mechi wanachechemea kutokana na kuumia katika moja ya harakati za kuipigania klabu yao.
    Matukio haya yaliyotokea siku nne kabla ya mechi ya kwanza na Cape Verde mjini Praia dhahiri yalikuwa kengere za hatari masikioni mwa Watanzania – na labda wapo wanaoweza kupuuza kwa kudhani Kakolanya na Dante si wachezaji muhimu sana Taifa Stars kwa sababu wote hawaanzi kwa sasa.
    Lakini yaliyowatokea yangeweza kuwatokea hata wachezaji wengine hao wanaotarajiwa kuanza, kwani Jumamosi kipa Aishi Manula, beki Shomari Kapombe na kiungo Jonas Mkude wote waliichezea klabu yao, Simba SC ikishinda 2-1 dhidi ya African Lyon hapo hapo Uwanja wa Taifa.
    Moja kati ya miaka ambayo Tanzania ilikuwa na timu nzuri ya taifa ni 1980, ikijimuisha mseto wa vijana walioibuliwa miaka hiyo na wakongwe walioanza kucheza tangu miaka ya 1970 katikati, wakiwemo wale waliocheza AFCON ya mwaka 1980 nchini Nigeria.
    Katika kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1982, Taifa Stars ilianzia ugenini na Kenya Julai 5 mwaka 1980 na bahati mbaya ikafungwa 3-1, lakini mchezo wa marudiano Julai 19 Harambee Stars wakapigwa 5-0 Dar es Salaam.
    Raundi ya pili Taifa Stars ikakutana na Nigeria na mechi ya kwanza Desemba 6 mjini Lagos ikamalizika kwa sare ya 1-1, hivyo Tanzania ikaelekeza nguvu kwenye mchezo wa marudiano nyumbani ishinde iingie Raundi ya Tatu ya mchujo, ambako ingebakiza kigingi kimoja tu kwenda Hispania zilikofanyika Fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1982.   
    Timu iliporejea Dar es Salaam ilikuwa ina wiki mbili kabla ya kurudiana na Super Eagles ambazo zilikuwa nyingi kwa maandalizi, kuwapa fursa makocha kupitia mapungufu yaliyojitokeza kwenye mechi ya kwanza na kuweka mkakati madhubuti wa kiushindi.
    Badala yake timu ilionekana kuwa na programu ya kawaida mno ya mazoezi na mbaya zaidi wachezaji wakaruhusiwa kwenda kuzitumikia klabu zao katika mechi ya Kombe la CCM baina ya Pan Africans na Yanga SC ambazo zilikuwa timu bora mno wakati huo na kwa pamoja na Simba, ndizo zilikuwa zinatoa wachezaji wengi Taifa Stars. 
    Beki chaguo la kwanza, tegemeo na Nahodha wa Taifa Stars wakati huo, Leodegar Tenga wa Pan Africans aliyeongoza vyema safu ya ulinzi kwenye mechi ya kwanza na Nigeria Uwanja wa Surulele akaumia kwenye mchezo huo baada ya kugongana na mshambuliaji mkongwe wa Yanga, Kitwana Manara. 
    Hiyo ilitokea kama siku tano kabla ya mechi na maumivu ya Tenga yalikuwa makubwa, ikabidi mchezo wa marudiano acheze beki chipukizi, Isihaka Hassan na matokeo yake Taifa Stars ikachapwa 2-0 Desemba 20 mwaka 1980 Uwanja wa Taifa na ndoto za Kombe la Dunia zikafia hapo.
    Na ni kwenye mechi hiyo Isihaka alipata jina la utani Chukwu, kwani alishindwa kumdhibiti mshambuliaji hatari wa Nigeria, Christian Chukwu aliyefunga mabao yote ya Super Eagles siku hiyo Uwanja wa Taifa langoni yupo Juma Pondamali ‘Mensah’, sasa kocha wa makipa wa Yanga.  
    Ni kosa kubwa lililofanywa na Chama cha Soka Tanzania (FAT), wakati huo Mwenyekiti alikuwa Alhaj Said El-Maamry, Ofisa Mstaafu wa Jeshi la Polisi, Mwanasheria na Wakili ambalo likaigharimu Taifa Stars.
    Hapana shaka makosa ya aina hii yanapaswa kuchukuliwa kama fundisho ili yasije kurudiwa – kwa vongozi wa sasa wa soka, akina Wilfred Kidau wanaoongoza kupitia google hawawezi kuwa wanayajua haya na hawawezi kuona umuhimu wake bila kusoma makala kama hizi.
    Lilikuwa kosa kubwa wachezaji wateule wa Taifa Stars kuondolewa kambini kwenda kuzitumikia klabu zao, wakati wamekiwshaingia kwenye programu za kocha kwa ajili ya mechi mbili dhidi ya Cape Verde.
    TFF iamue, kama dhamira kuu ni kwenda Cameroon tukubaliane kama Taifa kuipa kipaumbele timu ya taifa na inapokuwa kambini, wachezaji waelekeze fikra na nguvu zao Taifa Stars tu.
    Na kwa sababu kanuni zipo wazi, kwamba timu zenye wachezaji kuanzia watano timu ya taifa, mechi zao huahirishwa na chini ya hapo wanaendelea na Ligi, basi kosa kama lililofanyika mwishoni mwa wiki lisirudiwe. Mungu ibariki Taifa Stars. Mungu ibariki Tanzania. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YALIKUWA MAKOSA MAKUBWA KUWATOA WACHEZAJI KAMBINI TAIFA STARS KWENDA KUZICHEZEA KLABU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top