• HABARI MPYA

  Friday, October 19, 2018

  RAIS DK. MAGUFULI ASEMA ALITAKA AUNDE TIMU IMARA YA TAIFA JESHINI BAADA YA KUCHOSHWA NA MATOKEO MABAYA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli amesema kwamba alitaka kuunda timu imara ya taifa jeshini iandaliwe vizuri kuiletea nchi kwenye mashindano ya kimataifa.
  Akizungumza Ikulu mjini Dar es Salaam leo kabla ya kupata chakula cha mchana na wachezaji wa Taifa Stars, Rais Dk. Magufuli amesema kwamba mpango huo ameusitisha kutokana na matokeo mazuri ya Taifa Stars hivi sasa.   
  Wachezaji wa Taifa Stars wakiongozwa na Kocha wao, Mnigeria Emmanuel Amunike leo wamekula chakula cha mchana na Rais Magufuli Ikulu baada ya mwaliko wa kiongozi huyo mkuu wa nchi kufuatia ushindi wa 2-0 dhidi ya Cape Verde Jumanne kwenye mechi ya Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani nchini Cameroon. 
  Rais alisema mara baada ya kuingia madarakani na kuona timu zote hazifanyi vizuri, alifirikia kuchukua timu za wanajeshi achague wanajeshi wacheze mpira tu na wakikosea waadhibiwe kijeshi hadi siku moja ipatikane timu imara ya taifa. 

  Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli akikabidhi Sh. Milioni 50 kwa viongozi wa TFF leo Ikulu mjini Dar es Salaam

  Hata hivyo, Rais Magufuli amesema kwamba mwelekeo mzuri wa sasa wa timu ya Taifa umeanza kumpa matumaini, na hasusan baada ya ujio wa kocha Mnigeria, Amunike ambaye enzi zake alikuwa winga machachari wa timu yake ya taifa na klabu ya Barcelona ya Hispania.
  Rais Magufuli amesema kwamba Taifa Stars ilipofungwa 3-0 na wenyeji Cape Verde Oktoba 12 mjini Praia alisononeka mno na hata ilipokuja kushinda 2-0 kwenye mchezo wa marudiano Oktoba 16 hakufurahi sana kwa sababu bado ilizidiwa bao moja. 
  “Mmezidiwa moja. Niliwashangaa hata waliokuwa wanashangilia. Lakini angalau mwelekeo upo, ndiyo maana nikasema ngoja niwaite nisikilize changamoto zao na kama kiongozi niweze kuwasaidia,”amesema.
  Rais Magufuli alisema kwamba awali alisikitika mpango wake wa kutoa ndege ya Serikali iipeleke timu ya taifa Cape Verde uliposhindikana kwa sababu Uwanja wa Ndege wa Praia ni mdogo na ndege ya Dream Liner isingeweza kutua, lakini baada ya kipigo cha 3-0 akasema afadhali hakutoa ndege hiyo.
  Rais Magufuli ambaye aliichangia Taifa Stars Sh. Milioni 50 kusaidia maandalizi ya mchezo ujao ugenini dhidi ya Lesotho, alisema kwamba Watanzania wamechoka kuwa wasindikizaji na sasa wanataka kufurahia matokeo mazuri na huu ndiyo wakati wa mabadiliko kwa sababu timu ina kocha Amunike.
  Na akawaasa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutomuingilia kocha katika upangaji wa timu ili lawama ziende kwake iwapo matokeo hayatakuwa mazuri, ingawa pia aliwataka vijana wajitume na kuwasihi wakitaka kuwa wachezaji wazuri lazima waachane na pombe na anasa zote. 
  Rais akwaambia viongozi wa TFF kuhakikisdha Sh. Milioni 50 za maandalizi kuelekea mchezo na Lesotho alizowapa wanazitumia vizuri na si kuweka idadi kubwa ya viongozi wa kusafiri kuliko wachezaji.
  “Nitashangaa sana viongozi wakiwa wengi kuliko wachezaji, huwa wanakwenda wengi na wanajipa vyeo sijui Mshauri, sijui nani,”. 
  Rais Magufuli amesema pia kwamba atafurahi sana Taifa Stars ikifuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afruka (AFCON) atachukia wakarudi na sababu baada ya kufungwa, kwania vita iliyopo mbele ni ya kushinda, hakuna sababu.
  Akawageukia wachezaji wa timu hiyo na kuwataka kuweka kando tofauti ya klabu zao na kwenda Lesotho kuchezeni kama timu badala ya kuweka mbele maslahi binafsi ya klabu zao, kwani wakicheza na kufuzu AFCON watakuwa wamefanya kitu kikubwa na kujiengea heshima isiyofutika.
  “Tulipata uhuru tukiwa watu Milioni 10 leo tupo watu Milioni 55, aibu kubwa watu Milioni 55 tunashindwa kupata wachezaji 11 wanaoweza kuwaletea Kombe hata la Afrika, hicho huwa kinanisosnonesha. Naamini Watanzania wengi wamekata tamaa kushabikia timu za ndani,”amesema na kuongeza.
  "Mimi nilicheza mpira kuanzia nikiwa form one (kidato cha kwanza) mpaka form three (kidato cha nne), nilikuwa nacheza forward (mshambuliaji) na baadaye nikahamia kuwa golikipa, nilipoanza kuvaa miwani ugolikipa nao ukanishinda kwa sababu nilijua miwani itavunjika," alisema Rais Magufuli.
  Aidha, Rais Magufuli amesema kwamba yeye si shabiki wa timu nchini, kwa sababu kila timu aliyojaribu kuisapoti mwishowe ilifanya. 
  “Niseme kwa uwazi kwamba mimi napenda michezo, lakini siyo shabiki wa timu yoyote kwa sababu kila timu ambayo niliipenda, ikijitahidi ikakaribia mwisho, inashindwa, na mimi sipendi kushindwa,”alisema Rais Magufuli.
  Rais Magufuli alisema kwamba Tanzania inasikitisha kuona ilishiriki AFCON mara ya kwanza na ya mwisho mwaka 1980, enzi za utawala wa Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (sasa marehemu) na tangu haijaingia tena.
  “Tunapongezana kwa vikombe vya ovyo ovyo, mara mnaitwa bungeni, mara wapi, wanawapa viburi, lakini kiukweli hatufanyi vizuri,” amesema.
  Rais Magufuli pia alionyesha kukerwa na viongozi wasio waadilifu ambao wameiponza nchi kukosa fedha za msaada kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) zaidi ya dola za Kimarekani Miloni 3.
  “Zile fedha badala ya kusaidia wachezaji, zinaliwa na watu ambao hata hawaingii uwanjani. Sitaki nizungumzie sana, kwa sababu masuala mengine yapo mahakamani, viongozi wa michezo katika kipindi fulani hapa, walikuwa wa ovyo. Wanahangaika kupata nafasi wanahonga sana, wakishapata ni kwenda kurudisha zile fedha,”amesema.
  Rais Magufuli amesema kwamba matumizi mabaya ya fedha hayafanywi na viongozi wa TFF pekee, bali hata kwenye klabu nako ni hivyo na kwamba hivyo vitu vimekuwa vikiwakatisha tamaa Watanzania. 
  “Nitoe wito kwa Waziri na watendaji wote wa Wizara, lazima muwe wakali kwa watu ambao wanakaa tayari kufuja fedha. Lazima viwanja vyote vya michezo vitumie tiketi za elektrioniki, ili pia serikali ipate fedha zake,”amesema.
  Awali ya hapo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Dk. Augustine Mahiga alisema kwamba Taifa Stars inawakilisha Diplomasia ya Watu kwa Watu, hivyo inapofanya vizuri inaitanagza nchi.
  Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe alisema kwamba kipigo 3-0 kutoka nchini Cape Verde kiliwanyong’onyesha watu wengi kuliko hata Taifa Stars ilipofungwa 7-0 Algeria, kwa sababu hii ni Tanzania mpya ya ushindi na ndiyo maana mechi ya marudiano vijana walijituma sana na kushinda. 
  Naye Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Leodegar Tenga alisema kwamba Taifa Stars inahitaji ponti tatu za Lesotho ili kufuzu tena AFCON tangu 1980 kipindi ambacho wachezaji wote wanaounda timu ya taifa ya sasa walikuwa hawajazaliwa.
  Rais wa TFF, Wallace Karia alisema kwamba uongozi wake umewekeza nguvu zake katika maendeleo ya timu za taifa kuhakikisha zinafanya vizuri, lakini wanakabiliwa na changamoto kubwa ni fedha kwa sababu hawana udhamini wa kutosha.
  Kocha Amunike alisema anawaamini vijana wake wanaweza kuirejesha Tanzania kwenye ramani ya soka Afrika baada ya miaka 38 kwa sababu, wakifuzu AFCON itawajengea heshima kubwa na kukumbukwa daima.
  “Mkifuzu afcon nchi haiwezi kuwasahau, si kuhusu fedha. Ni heshima. Kuna hadithi ya Tanzania haijaenda AFCON kwa miaka 38, ni matarajio mtaweka historia mkifuzu. Na tukifuzu hautendi Cameroon kukamilisha idadi, tutakwenda kushindana,” alisema.

  Wachezaji wa Taifa Stars wakiwa Ikulu mjini Dar es Salaam leo

  Kaimu Bahodha, Erasto Edward Nyoni pamoja na kumkabdhi jezi Rais Magufuli, bukta na beji pia aliahidi watakwenda kupigana wapate tiketi ya kwenda Cameroon mwakani.  
  “Tumejisikia faraja kuwa hapa, hatuna maneno mengi sana zaidi ya kukupa shukrani. Hili ni deni kubwa, tutapambana tufanye vizuri mechi ijayo ili tufuzu AFCON,”alisema.
  Baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Cape Verde, Taifa Stars sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi L, ikifikisha pointi tano baada ya kucheza mechi nne, ikifungwa moja na sare mbili. 
  Uganda ambayo siku hiyo iliifunga tena Lesotho 2-0 mjini Maseru, ndiyo inaongoza kundi hilo kwa pointi zake 10 za mechi nne, wakati Cape Verde inabaki na pointi zake nne katika nafasi ya tatu. Lesotho ndiyo inashika mkia kwa pointi zake mbili.   
  Taifa Stars itasafiri kuifuata Lesotho mwezi ujao kabla ya kukamilisha mechi za Kundi L kwa kumenyana na Uganda Machi mwakani, miezi miwili tu kabla ya kuanza kwa AFCON ya mwakani. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: RAIS DK. MAGUFULI ASEMA ALITAKA AUNDE TIMU IMARA YA TAIFA JESHINI BAADA YA KUCHOSHWA NA MATOKEO MABAYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top