• HABARI MPYA

  Jumatano, Oktoba 24, 2018

  OKWI, CHAMA, KWASI NA SALAMBA WOTE WAFUNGA SIMBA SC YAIKANDAMIZA ALLIANCE FC 5-1 TAIFA

  Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
  MABINGWA watetezi, Simba SC wamepata ushindi wa kishindo baada ya kuichapa 5-1 Alliance FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Ushindi huo unaifanya Simba SC ifikishe pointi 20 baada ya kucheza mechi tisa na kupanda hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, sasa ikiziwa pointi nne na vinara, Azam FC ambao hata hivyo wamecheza mechi moja zaidi.
  Watani wao wa jadi, Yanga SC wanafuatia kwa pointi zao 19 na kesho watacheza mechi yao ya nane kwa kumenyana na KMC Saa 1:00 usiku Uwanja wa Taifa.
  Mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi alifunga bao la kwanza dakika ya 10 kwa kichwa akimalizia pasi ya kocha baada ya krosi ya beki Mghana, Nicholas Gyan baada ya kona fupi kutoka upande wa kulia.

  Kiungo Hassan Dilunga akibusu viatu vya Clatous Chama baada ya Mzambia huyo kufunga bao la tano. Wengine kulia ni Shomari Kapombe na Emmanuel Okwi

  Beki Mghana, Asante Kwasi akaifungia Simba SC bao la pili dakika ya 30, kabla ya Okwi kufunga tena dakika ya 62 akimalizia krosi ya Nahodha John Bocco iliyompita kipa mfupi wa Alliance FC, Kelvin Richard.
  Adam Salamba akaifungia Simba SC bao la nne dakika ya 70 akimalizia mpira uliookolewa kipa Kelvin Richard baada ya shuti la kiungo Mzambia, Clatous Chama.
  Mzambia huyo, Chama akakamilisha shangwe za mabao za SImba SC kwa kufunga bao zuri la tano dakika ya 87 baada ya kuwapangua wachezaji wa Alliance FC kabla ya kufumua shuti lilimpota kipa Richard.        
  Zabona Khamis akaifungia Alliance FC bao la kufutia machozi dakika ya 87 akitumia mwanya wa wachezaji wa Simba SC kuzubaa baada ya kupata bao la tano. 
  Ligi Kuu itaendelea kesho Mbeya City wakiwa wenyeji wa Mwadui FC ya Shinyanga Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya Saa 8:00 mchana, Stand United wakiwakaribisha Mtibwa Sugar ya Morogoro Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Ndanda FC wakiwakaribisha Biashara United ya Mara Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, Mbao FC wakiwa wenyeji wa  Lipuli FC ya Iringa zote Saa 10:00 jioni.
  Mechi za katikati ya wiki zitakamilishwa kwa mchezo baina ya wana Dar es Salaam watupu, KMC FC ya Kinondoni dhidi ya Yanga SC ya Kariakoo, Manispaa ya Ilala iliyotapakaa nchi nzima ambao utaanza Saa 1:00 usiku Uwanja wa Taifa.
  Kikosi cha Simba SC leo kilikuwa; Aishi Manula, Nicholas Gyan/Shomari Kapombe dk46, Asante Kwasi, Juuko Murshid, Pascal Wawa, Said Ndemla, Mohammed ‘Mo’ Ibrahim/Hassan Dilunga dk61, Clatous Chama, Adam Salamba/Meddie Kagere dk75, John Bocco na Emmanuel Okwi.
  Alliance FC; Kelvin Richard, Israle Patrick, Hance Masoud, Wema Sadock, Geoffrey Luseke, Juma Nyangi, Dickson Ambundo, Balama Mapinduzi/Martin Kiggi dk89, Michael Chinedu/Juhudi Philemon dk61, Jamal Mtegeta/Zabona Khamis dk80 na Siraj Juma.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: OKWI, CHAMA, KWASI NA SALAMBA WOTE WAFUNGA SIMBA SC YAIKANDAMIZA ALLIANCE FC 5-1 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top