• HABARI MPYA

  Jumanne, Oktoba 30, 2018

  MBAO FC CHUPUCHUPU KUPIGWA TENA KIRUMBA, YACHOMOA DAKIKA 10 ZA MWISHO SARE 2-2 NA MBEYA CITY

  Na Mwandishi Wetu, MWANZA
  TIMU ya Mbao FC leo imeponea chupuchupu kupoteza mechi ya pili mfululizo nyumbani, baada ya kulazimisha sare ya 2-2 na Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Huo unakuwa mchezo wa sita mfululizo kucheza bila ushindi kwa Mbao FC iliyoanza vizuri msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara hadi kuwafunga na mabingwa watetezi, Simba SC.
  Mbao FC ya kocha Amri Said ‘Stam’ ambayo mechi iliyopita ilifungwa 3-1 na Lipuli FC hapo hapo Mwanza, hadi mapumziko leo ilikuwa imekwishachapwa 1-0, bao la Mbeya City likifungwa na mshambuliaji wake hodari, Iddi Suleiman Nado dakika ya 11.

  Mbao FC leo imeponea chupuchupu kupoteza mechi ya pili mfululizo nyumbani

  Na dakika tatu tu baada ya kuanza kipindi cha pili, Mbeya City ya kocha Mrundi, Ramadhani Nswanzurimo ikapata bao la pili, lililofungwa na kinara wake wa mabao, Eliud Ambokile dakika ya 48.
  Lakini mtokea benchi, Evarigestus Mujwahuki akaja kuwapokonya ushindi Mbeya City baada ya kuisawazishia mabao yote Mbao FC dakika za 83 na 90 na ushei.
  Mara ya mwisho Mbao FC ilishinda Septemba 24, mwaka huu 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons uwanja wa CCM Kirumba na baada ya hapo imecheza mechi sita bila ushindi, ikiwemo ya leo.
  Ilitoa sare ya 1-1 na Coastal Union ya Tanga Septemba 28, ikafungwa 1-0 na Ruvu Shooting Oktoba 1 na 2-0 na Yanga SC Oktoba 7, zote ugenini kabla ya kutoa sare ya 0-0 na kufungwa 3-1 na Lipuli mjini Mwanza.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MBAO FC CHUPUCHUPU KUPIGWA TENA KIRUMBA, YACHOMOA DAKIKA 10 ZA MWISHO SARE 2-2 NA MBEYA CITY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top