VIGOGO, Simba SC wameibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji, Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara mchana wa leo Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee, winga kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Elie Mpanzu Kibisawala dakika ya 44 akimalizia kazi nzuri ya kiungo mkongwe, Mzambia Clatous Chota Chama.
Kwa ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi 64 katika mchezo wa 27 na kurejea kileleni mwa Ligi Kuu, ikiwazidi pointi moja mabingwa watetezi, Yanga SC ambao pia wana mchezo mmoja mkononi na kesho wanacheza na Fountain Gate Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha.
Kwa upande wao Mbeya City baada ya kupoteza mchezo huo wanabaki na pointi zao 25 kufuatia kucheza mechi 27 sasa – wakiendelea kushika nafasi ya 14 kwenye ligi ya timu 16 mwisho wa msimu timu mbili zitashuka Daraja moja kwa moja.
Timu nyingine mbili zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.
Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu kutoka Ligi ya Championship katika mechi nyingine mbili za mchujo nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ndiye atacheza Ligi Kuu msimu ujao.



.png)
0 comments:
Post a Comment