• HABARI MPYA

  Jumapili, Oktoba 28, 2018

  WANARIADHA WA TANZANIA BARA WATAMBA MBIO ZA KILOMITA 10 ZA KMKM ZANZIBAR

  Na Makame Mshenga, ZANZIBAR
  WAKIMBIAJI kutoka Tanzania Bara, wameibuka washindi wa nafasi zote tatu za juu kwa wanawake na wanaume katika mbio za kilomita kumi zinazoandaliwa na Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo Zanzibar, ‘KMKM 10 KM RACE.’
  Mashindano hayo ya nne tangu yalipoasisiwa mnamo mwaka 2016, yamerindima leo Oktoba 28, 2018 yakianzia makao makuu ya KMKM Kibweni kuzungukia Saateni, Malindi, Mkunazini, Michenzani, Miembeni, Kilimani na kumalizikia viwanja vya Maisara mjini Zanzibar.
  Mbali na mbio hizo kuu za kilomita kumi, pia kulikuwa na michuano ya aina mbalimbali iliyoshirikisha watu wa makundi tafauti, wakiwemo wazee wanawake na wanaume, vijana, watoto, wanafunzi pamoja na watu wenye ulemavu wa viungo na akili, ikiwemo kufukuza kuku, mbio za magunia, kuvuta kamba na mingine kadhaa.
  Kwa upande wa wanaume, walionyakua ushindi katika mtifuano wa kilomita kumi, ni Faraja Lazaro kutoka Arusha aliyetimka kwa dakika 29:37:60, akifuatiwa na Fabian Nelson kutoka Arusha (30:05:00) na wa tatu ni Nelson Priva (JKT) ambaye alitumia dakika 30:18:50.
  Waliotamba kufukuza upepo kwa wanawake kilomita kumi, ni Jacquline Juma 35:51:55 (JWTZ), Amina Mohammed 36.19,80 (JKT) na Angelina John kutoka Arusha ambaye alikimbia kwa dakika 36:54:36.
  Zawadi za aina mbalimbali zikiwemo pesa taslim zilikabidhiwa kwa washindi wote pamoja na washiriki wengine, kutoka kwa mgeni rasmi, Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Khalid Salum Mohammed.
  Viongozi wengine waliokabidhi zawadi ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma ‘Mabodi’, Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo.
  Wengine ni Wakuu wa Wilaya ya Kaskazini B, Kusini, Magharibi A na wengine kadhaa.
  Akizungumza na wanamichezo na wananchi waliohudhuria kabla kukabidhi zawadi na kuyafunga rasmi mashindano hayo, Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Khalid Salum Mohammed, aliupongeza uongozi wa KMKM kwa kubuni na kuyaendeleza mashindano hayo.
  Dk. Khalid alieleza kuwa, hatua hiyo ni muhimui klwani ni ueexzahi wa Ilani ya CCM na sera ya michezo Zanzuibvar, zinazohimiza wananchi kushirki michezo kwa ajili ya kujenga afya zao na pia kudumisha umoja, mapenzi na mshikamano miongoni mwao.
  Aidha, alieleza kuwa, katika dunia ya sasa, michezo imetoka kuwa sehemu ya burudani pekee,  na kuwa ajira inayoweza kuyabadilisha maisha ya washiriki iwapo itaendeshwa kwa weledi, umahiri na dhamira ya kufanya vyema.
  Alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi mahiri wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein, inaendelea kuzitatua changamoto zote zinazoikabili sekta ya michezo ili vijana waweze kushiriki kwa ufanisi, ikiwemo mkakati wa kuhakikisha inajenga viwanja vya kisasa katika kila wilaya Unguja na Pemba.
  Mapema, akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa kikosi cha KMKM, kiliamua kuyaendeleza mashindano hayo sio tu kwa kuwafurahisha wananchi, bali pia kikilenga kujenga mashirikiano kati yake na jamii.
  Aidha kujenga imani kwa jamii kwamba KMKM sio tu kikosi cha ulinzi pekee, bali pia ni kiungo muhimu cha michezo hapa nchini, ikizingatiwa kuwa ni ajira, na ndiyo maana wamekuwa wakishirikisha makundi mbalimbali, wakiwemo watu wenye ulemavu, vijana , wanawake wazee na kuanzia mwaka huu, watoto wenye umri wa miaka 12.    
  Wafadhili mbalimbali wa michuano hiyo walitunukiwa vyeti kutambua mchango wao, ambao ni pamoja na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa Zanzibar, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Zanzibar Quality Tailoring Ltd, na wadau wengine mbalimbali.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: WANARIADHA WA TANZANIA BARA WATAMBA MBIO ZA KILOMITA 10 ZA KMKM ZANZIBAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top