• HABARI MPYA

  Jumatatu, Oktoba 29, 2018

  MWADUI FC WAWATWANGA WAPINZANI WAO WA SHINYANGA NA KUANZA KUJINASUA MKIANI LIGI KUU

  Na Mwandishi Wetu, SHINYANGA
  TIMU ya Mwadui FC imeanza kujiinua kutoka mkiani baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Stand United katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
  Ahsante za kutosha kwa mfungaji wa bao hilo pekee, Ibrahim Irakoze dakika ya 27 na kwa ushindi huo kwenye mechi ya wapinzani wa mkoa mmoja, Mwadui FC inafikisha pointi tisa baada ya mechi 11 na kupanda hadi nafasi ya 19 kutoka ya 19 kwenye ligi ya timu 20.
  Stand United yenyewe baada ya kupoteza mchezo wa sita wa msimu, ikiwa imeshinda mara nne na sare mbili, inabaki na pointi zake 14 za mechi 12.

  Mechi nyingine ya Ligi Kuu iliyochezwa leo, African Lyon imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Biashara United ya Musoma mkoani Mara Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
  Na ni wageni, Biashara walitangulia kwa bao la Lambele Jerome dakika ya 59, kabla ya beki Ismail Gambo anayecheza kwa mkopo kutoka Azam FC kuisawazishia Lyon dakika ya 70.
  African Lyon inaangukia nafasi ya 19 baada ya sare hiyo ikijiongezea pointi moja na kufikisha nane baada ya kucheza mechi 12 na Biashara inapanda hadi nafasi ya 18 ikifikisha point inane pia baada ya kucheza mechi 11.
  Alliance FC ya Mwanza sasa ndiyo inazibeba timu nyingine zote 19 katika Ligi Kuu kwa sasa, ambayo kileleni ipo Azam FC yenye pointi 27 za mechi 11 ikifuatiwa na Simba SC pointi 23 za mechi 10 na Yanga SC pointi 22 mechi nane.
  Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi mbili, Mbao FC wakiwakaribisha Mbeya City Saa 10:00 jioni Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza na Yanga SC wakiwa wenyeji wa Lipuli FC kuanzia Saa 1:00 usiku Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MWADUI FC WAWATWANGA WAPINZANI WAO WA SHINYANGA NA KUANZA KUJINASUA MKIANI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top